1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Italia: Uchaguzi usiyo na mshindi

26 Februari 2013

Italia inakabiliwa na mkwamo wa kisiasa, baada ya kutokuwepo na mshindi wa moja kwa moja katika uchaguzi uliyofanyika Jumapili na Jumatatu, na hivyo kuweka mashakani juhudi za kufufua uchumi wa taifa hilo.

https://p.dw.com/p/17llt
Zoezi la kuhesabukura likianza baada ya siku mbili za uchaguzi
Zoezi la kuhesabukura likianza baada ya siku mbili za uchaguziPicha: AFP/Getty Images

Ugumu wa maisha na rushwa

Kura nyingi za hasira zilizopigwa na raia waliochoshwa na hali ngumu ya kiuchumi na rushwa katika siasa, zimeliacha taifa hilo lenye uchumi wa tatu kwa ukubwa katika kanda inayotumia sarafu ya euro, likibaliwa na ombwe kubwa, baada ya kutotoa mshindi mwenye nguvu za kutosha kuunda serikali. Matokeo hayo ambayo yalivipa vyama vinavyoipinga sarafu ya euro zaidi ya asilimia 50 ya kura, na mafanikio ya kustaajabisha ya vuguvugu jipya lenye propaganda za umaarufu, vilitikisa masoko ya fedha duniani, na kusababisha hofu ya mgogoro mpya katika kanda inayotumia sarafu ya euro.

Pier Luigi Bersani, kiongozi wa muungano wa vyama vya mrengo wa kati-kushoto uliyoshinda katika baraza la chini la bunge.
Pier Luigi Bersani, kiongozi wa muungano wa vyama vya mrengo wa kati-kushoto uliyoshinda katika baraza la chini la bunge.Picha: Alberto Lingria/AFP/Getty Images

Kufuatia matokeo hayo sarafu ya pamoja ya Ulaya ilishuka dhidi ya dola ya Marekani na Yen ya Japan, huku masoko ya hisa ya Marekani yakishuhudia anguko kubwa zaidi katika siku moja tangu Novemba mwaka jana. Wakati zaidi ya asilimia 99 ya kura zikiwa imekwisha hesabiwa, matokeo yalionyesha muungano wa vyama vya mrengo wa kati-kushoto ukiwa na ushindi mdogo wa karibu kura laki moja na thelathini katika baraza la chini la bunge, zinazotosha kuupa udhibiti wa baraza hilo.

Lakini hakuna chama au muungano uliyoshinda kura za kutosha kuunda wingi katika baraza la Seneti, na hivyo kupelekea bunge la mseto, kinyume na matokeo imara ambayo Italia ilikuwa inayahitaji ili kuweza kushughulikia mdororo mkubwa wa kiuchumi, ukosefu wa ajira na deni kubwa la taifa. Matokeo hayo yalichochea hofu ya mgogoro mpya wa fedha wa Ulaya. Alessandro Tentori, mkuu wa viwango vya kimataifa wa Citigroup, alisema matokeo hayondiyo mabaya zaidi kwa mtizamo wa masoko, na kuongeza kuwa kuna uwezekano mkubwa wa kufanyika kwa uchaguzi mpya.

Silvio Berlusconi akipiga kura yake. Muungano wake umeshika nafasi ya pili.
Silvio Berlusconi akipiga kura yake. Muungano wake umeshika nafasi ya pili.Picha: REUTERS

Beppe Grillo na mapinduzi ya kisiasa

Lakini matokeo hayo yalikuwa na mafanikio ya kipekee kwa mchekeshaji kutoka Genoa Beppe Grillo, kiongozi wa vuguvugu la nyota 5, aliezunguka nchi katika kampeni yake ya kwanza akiwakosoa wanasiasakwa kuifkikisha Italia katika hali iliyomo sasa. Mafanikio yake yametimiza utabiri wa baadhi ya wachambuzi kuwa uchaguzi huo usiyotabirika na uliyofuatiliwa kwa karibu zaidi katika miaka kadhaa unaweza kuleta mapindizi ya kisiasa.

"Tumefurahi sana kwa sababu hii ni kama tsunami. Inastajabisha kwenda kupiga kura ukiwa na tabasamu na ukafurahia zoezi hilo. Watu wengi ambao walikuwa hawapiga kura kwa muda mrefu walituambia wanarudi kupiga kura na hilo limesaidia viguvugu letu," alisema Allisandro Di Battista, mgombea wa vuguvugu hilo akiufananisha ushindi wao na tufani ya tsunami. Grillo alipata karibu robo ya kura, kutoka asilimia 1.8 aliyolipatia vuguvugu lake katika jaribio lakwanza mwaka 2010.

Kibao cha fedheha kwa Bersani

Matokeo hayo yalikuwa kibao cha fedheha usoni mwa kiongozi wa muungano wa vyama vya mrengo wa kati-kushoto Pier Luigi Bersani, ambaye alipoteza uongozi wa asilimia 10 ya kura za maoni chini ya miezi miwili iliyopita dhidi ya muungano wa vyama vya mrengo wa kati-kulia unaoongozwa na tajiri Silvio Berlusconi.

Bersani alishindwa kuhudhuria mkutano wa waandishi wa habari baada ya matokeo kujulikana bayana. Naibu wake Enrico Letta, pamoja na waziri mkuu anaemaliza muda wake Mario Monti, walisema pande zinazohusika zinapaswa kuunda serikali ili kuepusha uchaguzi mwingine. Lakini matokeo hayo yanazua masuali kama hilo linawezekana.

Kiongozi wa vuguvugu la nyota tano Beppe Grillo, aliyeshika nafasi ya tatu.
Kiongozi wa vuguvugu la nyota tano Beppe Grillo, aliyeshika nafasi ya tatu.Picha: Giuseppe Cacace/AFP/Getty Images

Tajiri Berlusconi mwenye umri wa miaka 76 ambaye anakabiliwa na kashfa za ngono na rushwa, alishika nafasi ya pili katika kinyanganyiro cha baraza la seneti akiwa na takribani viti 117. Kura zote zikiwa karibu zimekamilika, muungano wa kati-kushoto ulitarajiwa kushinda jumla ya viti 121 katika seneti, Grillo 54 na Monti akiambulia viti 22. Wingi katika baraza la seneti ni viti 158.

Hatari ya uchaguzi mwingine

Wawekezaji wanahofia kurudi kwa mgogoro wa madeni uliyoipeleka kanda ya euro karibu na maafa na kumleta madarakani msomi Monti, akichukua nafasi ya Berlusconi mwaka 2011. Matokeo yanaonyesha zaidi ya nusu ya wapiga kura waliyachagua majukwaa ambayo sera zake zinapingana na kanda ya euro, ya Berlusconi na Grillo.

Serikali ya mrengo wa kati-kushoto ikiongoza peke yake au kwa kushirikiana na Mario Monti ilikuwa inatizamiwa na wawekezaji kama uthibitisho bora wa hatua za kukabiliana na mdororo mkubwa na ukuaji uliyotwama nchini Italia, ambayo ni muhimu kwa utulivu wa sarafu ya muungano. Lakini kushindwa kwa Monti licha ya kuungwa mkonona wafanyabiashara, na mtokeo yasiyoridhisha ya muungano wa vyama vya mrengo wa kati-kushoto, kunamaanisha kuwa hawana maseneta wa kutosha kuunda serikali hiyo.

Monti aliisaidia Italia kutoka katika mgogoro wa madeni wakati ambapo gharama za ukopaji zilikuwa zinapanda kwa kiwango cha kutisha Novemba 2011, lakini watalia wachache sasa hivi wanaomuona kama muokozi wa taifa hilo, linalokabiliwa na mdororo wa muda mrefu zaidi katika kipindi cha miaka 20. Vuguvugula Grillo liliendesha kampeni ya kuwavuta wapiga kura wenye hasira dhidi ya programu ya kubana matumizi ya Monti, na mlolongo wa kashfa.

Waziri mkuu anayemaliza muda wake Mario Monti.
Waziri mkuu anayemaliza muda wake Mario Monti.Picha: Gabriel Bouys/AFP/Getty Images

Berlusconi alitumia vizuri hasira za raia dhidi ya hatua za Monti za kubana matumizi, akimtuhumu kuwa kibaraka wa Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel, lakini katika maeneo mengi Grillo ndiye aliyenufaika zaidi kutokana na hasira za wananchi. Rais Giorgino Napolitano anatarajiwa kuwaita viongozi wa kisiasa kujadili namna ya kuunda serikali, lakini hili halitarajiwi hadi Machi 10 baada ya matokeo kuthibitishwa rasmi na kuitishwa bunge.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/rtre, afpe, ape
Mhariri: Daniel Gakuba