Italia na Malta zawajibika vifo vya wahamiaji
1 Oktoba 2014Kulingana na ripoti ya shirika hilo iliyotolewa jana jioni, wanamaji wa Italia na Malta walijivuta mno katika kuitikia wito wa msaada uliotolewa na boti hiyo iliyokuwa ikizama tarehe 11 Oktoba mwaka 2013, katika bahari ya Mediterania kwenye eneo ambalo liko chini ya operesheni za uokozi wa kisiwa cha Malta. Miongoni mwa wahamiaji wapatao 400 waliokuwa ndani ya boti hiyo iliyokwenda mrama, Malta iliweza kuokoa watu 147, huku Italia ikinusuru 39 tu. Inaaminika kuwa wahamiaji zaidi ya 200 waliobaki waliangamia baharini.
Ripoti hiyo Amnesty International inasema ni sahihi kutilia shaka iwapo kweli Italia na Malta zilichukua hatua kwa muda unaofaa, na kwa kutumia uwezo wao wote kuwaokoa watu hao. Na hapo linaibuka swali kwamba, je kucheleweshwa kwa shughuli za uokozi kwaweza kuwa kulichangia katika kuzama kwa boti hiyo?
Maswali yasio na majibu
Na hilo sio swali pekee ambalo Amnesty International inalo kuhusu majaliwa ya wahamiaji wanaotumia bahari ya Mediterania kutaka kuingia barani Ulaya. Mkuu wa shirika hilo barani Ulaya na Asia ya Kati John Dalhuisen anasema ni lazima sera ya Ulaya kuhusu wahamiaji hao ieleweke.
''Ulaya imejitayarisha kufanya nini, kuzuia idadi ya vifo vya baharini vya wakimbizi na wahamiaji inayozidi kuongezeka? Mwaka huu pekee wapatao 2,500 wamezama katikati mwa Mediterania, idadi jumla ya waliokufa kuanzia mwaka 2000, ni kati ya 20,000 na 25,000. Hizi ni takwimu za kutisha, za kutisha kabisa''. Amesema afisa huyo.
Ikirejea kwenye ajali ya Oktoba mwaka jana, ripoti hiyo inasema boti ya wahamiaji iliomba msaada wa dharura baada ya kushambuliwa kwa risasi na chombo cha Libya, lakini ilichukuwa masaa kati ya 5 na 6 kabla ya msaada huo kuwafikia. Inasema kwanza waliomba usaidizi kutoka Italia, wakaambiwa inawabidi kuita Malta iliyo karibu. Malta nayo ilijikokota katika kutoa msaada huo.
Lazima Ulaya iwajibike
John Dalhuisen wa Amnesty International anasema Ulaya inawajibika kufanya vyema zaidi kuliko kuwazuia wahamiaji kwenye ardhi yake.
Alisema, ''Kama jibu la Ulaya kuhusu mgogoro huu wa kibinadamu ni kuiziba mipaka yake, na kuwaacha wahamiaji waangamie, hiyo ni aibu kubwa sana, sana''.
Amnesty International imetoa wito kwamba uzembe huo wa Italia na Malta uchunguzwe, watakaopatikana na hatia washitakiwe, na fidia itolewe kwa familia za watu walioangamia katika mkasa huo.
Huku idadi ya wahamiaji wanaoyahatarisha maisha yao kuingia Ulaya kupitia bahari ya Mediterania ikizidi kupanda, mtu ambaye ameidhinishwa kuwa kamishna mpya wa Umoja wa Ulaya ahusikaye na masuala ya wahamiaji Dimitris Avramopoulos, amesema Ulaya lazima isimame bega kwa bega na Italia ambayo ni mlango wa wahamiaji hao kuingia barani Ulaya.
Amesema watu wanaochukua njia hiyo wose si magaidi na wahamiaji haramu, bali watu wenye sababu halali za kutafuta hifadhi, na kuongeza kuwa mzigo huo haupaswi kuachiwa nchi za Ulaya kusini kuubeba peke yao.
Mwandishi: Daniel Gakuba/dpae/rtre
Mhariri:Josephat Charo