1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Italia kumpata waziri mkuu

22 Mei 2018

Rais wa Italia anakutana na viongozi bunge la nchi hiyo kumjadili mwanasheria asiyefahamika sana aliyeteuliwa na muungano wa vyama vya siasa kali na wastani za mrengo wa kulia kuwa waziri mkuu.

https://p.dw.com/p/2y6Hh
Italien Giuseppe Conte soll neuer Ministerpräsident werden
Picha: picture-alliance/AP Photo/A. Carconi

Rais Sergio Mattarella anakutana na Spika wa Baraza la Wawakilishi Roberto Fico na Mkuu wa Seneti Elisabeth Alberti Casellati, muda huu kwenye kasri lake mjini Rome, lengo likiwa kumjadili profesa wa sheria, Giuseppe Conte, anayetazamiwa kuwa waziri mkuu.

Jina la msomi huyo wa sheria mwenye umri wa miaka 54 lilipendekezwa wakati wa mazungumzo kati ya Rais Mattarella na kiongozi wa Vuguvugu la Nyota Tano, Luigi Di Maio na mkuu wa chama cha kizalendo, Matteo Salvini. 

"Tumelitaja jina la Giuseppe Conte kwa Rais wa Jamhuri, aliandika Luigi Di Maio kwenye blogu rasmi ya Vuguvugu la Nyota Tano muda mchache baada ya kukutana na Rais Mattarella jioni ya jana, akimtaja mwanasheria huyo asiyefahamika kama kiini cha vuguvugu lao na ambaye hatokuwa mzigo kwa umma wa Italia.

Baadaye naye Salvini alithibitisha kuwa Conte alikuwa pia chaguo la chama chake cha kizalendo, League, kama kijulikanavyo, akimtaja kuwa mtaalamu wa urahisishaji, asiyependelea urasimu na anayependelea utawala usio mazonge, sifa ambazo alisema Salvini, zinatakiwa na wawekezaji walio wengi.

Umoja wa Ulaya wataka umakini

Belgien EU-Kommission Pressekonferenz Valdis Dombrovskis
Makamu Rais wa Kamisheni ya Ulaya, Valdis Dombrovskis.Picha: Reuters/E. Vidal

Hayo yanajiri wakati Makamu wa Rais wa Kamisheni ya Ulaya, Valdis Dombrovskis, akiitaka Italia kutekeleza sera madhubuti ya kibajeti, katika wakati huu ikiunda serikali mpya inayouleta pamoja mseto wa vyama vya siasa kali na siasa za wastani za mrengo wa kulia chini ya waziri mkuu mtarajiwa, Conte.

Akizungumza na gazeti la kibiashara la Ujerumani, Handelsblatt, makamu rais huyo wa kamisheni ya Ulaya amesema na hapa namnukuu: "Msimamo wetu ni kwamba ni muhimu kwa serikali ya Italia kubakia kwenye njia sahihi ya kutekeleza bajeti inayowajibika. Italia ni ya pili kwa kuwa na kiwango cha juu cha deni baada ya Ugiriki." Mwisho wa kumnukuu.

Deni la euro trilioni 2.3 la Italia ni asilimia 132 ya pato lake jumla la ndani, kikiwa ni kiwango cha juu kabisa ukiiondoa Ugiriki. Umoja wa Ulaya unabashiri kwamba deni la Ugiriki litaendelea kubakia hapo hapo kwa mwaka huu mzima, ambapo ni zaidi ya mara mbili ya ukomo wake wa kukopesheka wa asilimia 60. 

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman