1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Itali, Ureno na Uhispania zapinga pendekezo la Ujerumani kujenga kambi za kuwazuia wahamaji wasio halali Afrika Kazkazini.

Josephat Charo4 Oktoba 2004

Itali, Ureno na Uhispania zimesema pendekezo la Ujerumani kuwazuia wahamaji wasio halali kuingia katika mataifa ya umoja wa Ulaya kwa kuwaweka katika kambi zitakazoanzishwa Afrika Kaskazini, unatakiwa kufanyiwa uchunguzi zaidi.

https://p.dw.com/p/CHiN
Waziri wa mambo ya ndani wa Ujerumani, bwana Otto Schily.
Waziri wa mambo ya ndani wa Ujerumani, bwana Otto Schily.Picha: AP

Katika mkutano wa siku nne wa mawaziri wa mambo ya kigeni uliofanyika mjini Rome, Itali, Ufaransa iliunga mkono pendekezo la serikali ya Berlin la kuanzisha kambi Afrika Kazkazini, zitazotumiwa kuwazuia wahamaji wasio halali kuingia mataifa ya jumuia ya Ulaya. Lakini Itali, Ureno na Uhispania zimesema wazi mpango huo unahitaji kuchunguzwa kwanza kabla hatua yoyote kuchukuliwa.

Waziri wa mambo ya kigeni wa Itali, bwana Franco Frattini, aliwaambia waandishi wa habari kwamba ni mapema sana kufanya uamuzi kuhusu swala hilo, hasa ikizingatiwa kuwa mazungumzo hayo bado yako katika hatua za mwanzo. Aliongeza kusema ni jukumu la viongozi hao kuchunguza athari za mpango huo kwa maisha ya wahamaji na vipi haki zao zitakavyoathiriwa.

Waziri wa mambo ya kigeni wa Uhispania, Miguel Angel Moratinos, na waziri wa mambo ya nchi za kigeni wa Ureno, Antonio Monteiro, wote walisema halitakuwa jambo la busara kulitupilia mbali pendekezo hilo, bila kulifanyia uchunguzi kubaini ikiwa litakuwa na manufaa.

Itali itafaidika sana ikiwa mtiririko wa wahamaji utadhibitiwa, na tayari imeliunga mkono pendekezo hilo lililowasilishwa na waziri wa mambo ya ndani wa Ujerumani, bwana Otto Schilly.

Mamia ya wahamaji wanaotafuta maisha mazuri huwasili katika bandari za kusini mwa Itali kila wiki. Wengi wao hujaribu kuingia Ulaya kazkazini na huwa mikononi mwa watu wanaojihusisha na biashara ya uchukuzi wa binadamu.

Fratini alisema kuanzishwa kwa vituo vya kuwazuia wahamaji hao kunaweza kusaidia kuleta maendeleo katika mataifa wanakotoka. Lakini ikiwa kambi hizo zitaanzishwa pasipo kushughulikia matatizo yanayokabili mataifa ya wahamaji hao, maazimio ya mkutano wa Roma, hayatakuwa na maana yoyote.

Waziri wa mambo ya kigeni wa Ufaransa, Michel Barnier, alieleza msimamo wa serikali yake kuhusu pendekezo hilo, akisema kuna maswala mengi yanayohusiana na haki za binadamu, ambayo lazima yajadiliwe.

Ufaransa inataka kujua vipi mpango huo utakavyodhaminiwa na ikiwa utaheshimu haki za binadamu. Pia imetaka kujua ikiwa kambi hizo za wahamaji hazitawavutia wafanyabiashara wa uchukuzi wa binadamu, ambao hupata maelfu ya dola kwa kuwaingiza watu barani Ulaya, kwa njia isiyo halali.

Waziri wa mambo ya ndani wa Ujerumani, bwana Otto Schily, katika pendekezo lake kwa Umoja wa Ulaya, aliloliwasilisha kwenye mkutano uliofanyika mjini Scheveningen, Uholanzi, Ijumaa iliyopita, alisema Umoja wa Ulaya lazima ukabiliane kwa dharura, swala la wahamaji wasio halali, ambao huhatarisha maisha yao kila siku wakijaribu kuingia Ulaya kutoka Afrika Kazkazini, wakitumia madau madogo.

Makundi ya kutetea haki za binadamu pia yameeleza wasiwasi wao kuhusu uwezo wa kambi hizo kuwalinda wahamaji kikamilifu. Serikali ya Sweden imepinga pendekezo hilo na kuutaka umoja wa Ulaya kutafuta njia nyingine za kushughulikia matatizo ambayo ni sababu halisi za uhamaji.

Waziri wa mambo ya ndani wa Ubelgiji, bwana Patrick Dewael, amelipinga pendekezo hilo, akisema kambi hizo zitashughulikia asilimia kumi tu ya uhamaji unaondelea kwa sasa.

Katika mwaka wa 2003, Uingereza ililizamishwa kufutilia mbali pendekezo lake kama hilo, la kujenga vituo vya wahamaji nje ya Ulaya, baada ya kushurutishwa na Sweden na Ufaransa, ambazo zilisisitiza ni kinyume cha sheria za kimataifa. Bunge la Ulaya pia lilikataa mpango huo.