1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Istanbul: Uturuki inayalaumu mataifa ya Umoja wa Ulaya kutofanya zaidi dhidi ya Wakurd wa Chama cha PKK.

28 Oktoba 2007
https://p.dw.com/p/C7Bo

Waziri mkuu wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan, ameyalaumu mataifa ya Umoja wa Ulaya kwa kutofanya zaidi katika kupambana na harakati za Chama cha Wakurd cha PKK kinachoendesha mapigano huko Uturuki kutokea Kaskazini mwa Iraq. Alisema mataifa ya Umoja wa Ulaya hayawakamati wanachama wa PKK au kuwakabidhi kwa Uturuki. Uturuki mara kadhaa imeziomba nchi za Umoja wa Ulaya kufanya zaidi dhidi ya chama cha PKK ambacho Umoja wa Ulaya unakiona kuwa ni chama cha kigaidi. Bwana Erdogan alisema hayo baada ya kufanyika mazungumzo baina ya Uturuki na Iraq na ambayo yalimalizika bila ya kupatikana maendeleo kuhusu mapendekezo ya Iraq ya kusitisha mashambulio ya Chama cha PKK huko Uturuki kutokea ardhi ya Iraq. Uturuki imeonya kwamba haitostahamilia mashambulio zaidi na imekusanya majeshi yake mpakani. Mamia ya watu wamefanya maandamano katika miji ya Waturuki wakikilaani chama cha PKK na kutaka zichukuliwe hatua.