1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yatakiwa kuendeleza mchakato wa amani

19 Machi 2015

Umoja wa Mataifa umesema Israel inapaswa kuendelea na mchakato wa kutafuta amani ya Mashariki ya Kati, ili iweze kuendelea kutambuliwa kama nchi ya kidemokrasia.

https://p.dw.com/p/1Et84
Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu
Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin NetanyahuPicha: Reuters/Amir Cohen

Kauli hiyo imetolewa baada ya Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu kubadili msimamo wake kuhusu majadiliano ya kuundwa kwa taifa la Palestina, wakati wa kipindi cha mwisho cha kampeni.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon, ametoa wito huo baada ya chama cha Netanyahu cha Likud kushinda katika uchaguzi mkuu uliofanyika siku ya Jumanne. Wakati wa siku za mwisho wa kampeni, Netanyahu aliapa kutoruhusu kuundwa kwa taifa la Palestina na kwamba ataendelea na ujenzi wa makaazi ya Walowezi wa Kiyahudi.

Akizungumza kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York, Msemaji wa Umoja huo, Farhan Haq, amesema Ban ameupongeza ushindi wa Netanyahu na ameelezea matumaini yake kwamba kiongozi huyo ataunda haraka serikali mpya itakayozingatia maslahi na matakwa ya wapiga kura wote wa Israel.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-MoonPicha: Reuters/R. Sprich

''Katibu Mkuu anaamini kuwa mchakato wa kutafuta amani unaojumuisha pia kusitishwa ujenzi wa makaazi ya Walowezi, ndiyo njia pekee kwa Israel kuthibitisha kwamba ni nchi inayozingatia demokrasia,'' alisema Haq.

Kwa upande wake Balozi wa Israel kwenye Umoja wa Mataifa, Ron Prosor, amesema umoja huo unaweza usikubaliane na sera za serikali ya Israel, lakini ukweli uko wazi kwamba hakuna mjadala kuwa Israel ndiyo nchi pekee inayozingatia demokrasia katika Mashariki ya Kati.

Marekani yaapa kuendelea kutafuta amani Mashariki ya Kati

Ama kwa upande mwingine Marekani imeapa kuendelea na mchakato wa kutafuta amani ya Mashariki ya Kati na kuanzishwa kwa taifa la Palestina, lakini hata hivyo imekiri kuwa msimamo mkali wa Netanyahu alioutoa wakati wa kampenzi za uchaguzi, umeifanya nchi hiyo kutathmini upya mikakati yake.

Msemaji wa Ikulu ya Marekani, Josh Earnest, amesema kuwa maoni ya Rais Barack Obama ni suluhisho la kuwepo mataifa mawili, ambayo ndiyo yatawezesha kumaliza mvutano uliopo kati ya Israel na Palestina.

Kiongozi wa Umoja wa Kizayuni, Isaac Herzog
Kiongozi wa Umoja wa Kizayuni, Isaac HerzogPicha: Getty Images/AFP/C. Magen

Wakati huo huo, kiongozi wa Umoja wa Kizayuni, unaofata siasa za wastani za mrengo wa kushoto nchini Israel, Isaac Herzog, ambaye ameshika nafasi ya pili, amesema hatojiunga katika serikali ijayo ya Netanyahu, na amemshutumu kiongozi huyo kwa ubaguzi wa rangi. Akizungumza leo kwenye kituo kimoja cha redio, Herzog amesema ataendelea kubakia mpinzani ili aweze kuikosoa serikali mpya ya Netanyahu.

Herzog alizikosoa kampeni za Netanyahu akisema ziligusa masuala ya ubaguzi wa rangi, na ziligubikwa na uwongo, chuki na uadui. Matamshi ya Netanyahu yalikosolewa vikali na jamii ya Waarabu wa Israel na yalikemewa na Ikulu ya Marekani. Chama cha Herzog, kimejinyakulia nafasi ya pili katika uchaguzi huo mkuu wa Israel, baada ya kupata viti 24 vya bunge, huku chama cha Likud cha Netanyahu kikishinda kwa viti 30.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/RTRE,APE,AFPE
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman