1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yakosowa makubaliano ya Geneva

24 Novemba 2013

Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ameyataja makubaliano hayo kuwa ni "kosa la kihistoria." na Kuongeza kwamba kamwe hayatobadilisha nia ya Iran ya kutaka kumiliki bomu la Nyuklia

https://p.dw.com/p/1ANEH
Waziri mkuu Benjamin Netanjahu na aliyekuwa waziri wa ulinzi Schaul Mofas
Waziri mkuu Benjamin Netanjahu na aliyekuwa waziri wa ulinzi Schaul MofasPicha: Reuters

Rais wa Iran Hassan Rouhani ameyataja makubaliano ya nyuklia kati ya nchi yake na nchi zenye nguvu duniani kwamba yanatambuwa haki ya nchi yake kuwa na mpango wa atomiki kwa kuridhia nchi hiyo iendelee na shughuli zake za urutubishaji wa madini ya Urani kama ilivyokuwa huko nyuma.

Katika taarifa aliyoitowa leo (24.11.2013) kupitia kituo cha televisheni ya taifa, Rouhani amesema mazungumzo yatafanyika mara moja juu ya makubaliano kamili ya pande mbili, na kwamba nchi yake ina nia ya dhati ya kuyazingatia mara moja makubaliano hayo.

Aliweka wazi pia kwamba mafanikio ya mazungumzo ya nyuklia yametokana na muongozo uliotolewa na Kiongozi Mkuu wa Iran, Ayatollah Ali Khamenei.

Mawaziri wa nje,William Hague,Mohammad Javd Zarif,Guido Westerwelle na mkuu wa sera za nje wa EU Catherine Ashton
Mawaziri wa nje,William Hague,Mohammad Javd Zarif,Guido Westerwelle na mkuu wa sera za nje wa EU Catherine AshtonPicha: Reuters/Jean-Christophe Bott

Kilichomo kwenye makubaliano

Makubaliano hayo ya mwanzo yaliyofikiwa mjini Geneva yamepongezwa na Urusi. Waziri wake wa Mambo ya Nje Sergei Lavrov amesema ni hatua itakayozifaidisha pande zote.

Kwa mujibu wa makubaliano hayo Iran imekubali kuzuia mpango wake wa nyuklia angalau kwa miezi sita, wakati nchi zenye nguvu zikiahidi kuiondolea vikwazo kadhaa.

Aidha Iran imekubali kutowa nafasi kwa Shirika la Kimataifa la Kudhibiti Nishati ya Nyuklia (IAEA) kufanya ukaguzi mpana katika mitambo yake ya nyuklia, kitendo ambacho bila ya shaka kimeongeza hali ya kuaminiana iliyohitajika katika eneo la Ghuba na Mashariki ya Kati na kupunguza hofu juu ya mpango huo wa Iran

Msimamo wa Israel na Marekani

Hata hivyo, Israel haikupendezwa na hatua ya nchi zenye nguvu, huku Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu akiyataja makubaliano kuwa ni "kosa la kihistoria." Netanyahu ameuambia mkutano wa waandishi wa habari mjini Tel-Aviv kwamba awamu hiyo ya mwanzo ya makubaliano haitoifanya Iran kusimamisha kile ilichokiita nia ya kutengeneza silaha za nyuklia, lakini akaapa "kutokuiruhusu Iran" kuwa na silaha hizo.

Pamoja na kauli hiyo ya waziri mkuu, upande wa maafisa wa kijeshi na serikali ya Israel umekiri kwamba kulikuwa hakuna la kufanyika kuzuia makubaliano hayo mjini Geneva.

Israel lakini imesema itafanya kila iwezalo kuwa na ushawishi katika makubaliano ya mwisho ambayo yatajadiliwa katika kipindi cha miezi sita. Kimsingi taifa hilo la Kiyahudi lina amini kwamba Iran inajaribu kutengeneza bomu la nyuklia na katika kipindi cha wiki kadhaa kabla ya makubaliano ya Jumapili lilionya kwamba makubaliano yatakayofikiwa hayatoshelezi.

Rais Barack Obama wa Marekani
Rais Barack Obama wa MarekaniPicha: Reuters

Waziri wa Israel anayehusika na masuala ya ujasusi na ambaye miongoni mwa majukumu yake ni kufuatilia mpango wa nyuklia wa Iran, Yuval Steinitz, amesema makubaliano ya nchi zenye nguvu na Iran bado ni mabaya na yataifanya hali kuwa ngumu zaidi kuliko ilivyokuwa katika kupatikana suluhisho linalohitajika hapo baadaye.

Steinitz amesema ni hatua itakayoiweka Iran karibu na umiliki wa bomu huku akiifananisha hatua ya makubaliano hayo kuwa kama ile ya mwaka 2007 kati ya jumuiya ya kimataifa na Korea ya Kaskazini iliyoshindwa.

Mshirika wa karibu wa Israel, Marekani imeyaridhia matokeo ya mkutano wa Geneva ambapo taarifa iliyotoka Ikulu ya White House imeyataja makubaliano hayo ya nyuklia kama hatua ya mwanzo katika mazungumzo ya miezi sita. Rais Barack Obama amesema sasa Iran inapaswa kuonesha ukweli wa dhamira yake ya nyuklia kwa matumizi ya amani.

Lakini taarifa hiyo pia imebainisha kwamba vikwazo katika masuala muhimu kama mafuta, benki na fedha vitabakia na kusisitiza ikiwa Iran itakwenda kinyume na makubaliano yaliyofikiwa basi hatua ya nchi hiyo kupunguziwa vikwazo itabatilishwa.

Rais wa Umoja wa Ulaya Herman Van Rompuy (kushoto) na mkuu wa Tume ya Umoja huo Jose Manuel Barrosso
Rais wa Umoja wa Ulaya Herman Van Rompuy (kushoto) na mkuu wa Tume ya Umoja huo Jose Manuel BarrossoPicha: Georges Gobet/AFP/Getty Images

Kinachosemwa na Umoja wa Ulaya

Rais wa Umoja wa Ulaya Herman Van Rompuy amepongeza ujasiri ulioonyeshwa na Iran na nchi zenye nguvu Marekani, Ufaransa, Ujerumani, Uingereza, China na Urusi. Van Rompuy amesema ni muhimu hivi sasa kuhakikisha utekelezaji unazingatiwa kama inavyohitajika kwa mujibu wa makubaliano.

Mkuu huyo wa Umoja wa Ulaya ameelezea matumani yake kwamba kushughulikia kwa suala hili kutaleta mabadiliko makubwa katika eneo zima na duniani kwa ujumla, ambayo ameyataja ni kupunguwa kwa misuguano ya kisiasa pamoja na kuchangia kuleta hali ya kuaminiana na uungaji mkono wa hatua za kupunguza utapakazaji wa silaha za maangamizi makubwa.

Mwandishi: Saumu Mwasimba/AP/Reuters

Mhariri: Mohammed Khelef