1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yaendelea kupambana vikali na kundi la Hezbollah

13 Oktoba 2024

Mapambano yameendelea nchini Lebanon ambapo kundi la wanamgambo la Hezbollah limesema limewashambulia kwa makombora wanajeshi wa Israel waliokuwa wakijaribu kuingia katika kijiji cha kusini cha Maroun al-Ras.

https://p.dw.com/p/4ljLP
Uharibifu nchini Lebanon kufuatia mashambulizi ya Israel
Uharibifu nchini Lebanon kufuatia mashambulizi ya IsraelPicha: dpa/AP/picture alliance

Mamlaka ya Lebanon imesema mashambulizi ya anga ya Israel yameharibu kabisa msikiti mkongwe unaotajwa kuwa na karibu miaka 100 katikati mwa kijiji cha Kfar Tibnit, eneo la kusini. Fuad Yassin, Meya wa kijiji hicho kilichopo takriban kilomita nane kutoka mpakani, amesema wamepoteza eneo pendwa lililokuwa likiwaleta watu pamoja.

Soma pia: Serikali ya Lebanon yatoa wito wa usitishwaji mapigano kati ya Israel na Hezbollah

Aidha, Shirika la Msalaba Mwekundu la Lebanon limesema wahudumu wake wa afya wamejeruhiwa kufuatia mashambulizi ya leo Jumapili huko Sirbin. Tangu Israel ilipoanza kupambana na Hezbollah kwa mwaka mmoja sasa, watu zaidi ya 2,250 wameuawa na maelfu ya wengine wameyahama makazi yao.