1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroMamlaka ya Palestina

Israel yaendelea kuushambulia ukanda wa Gaza

9 Juni 2024

Vikosi vya Israel vimeyapiga maeneo ya katikati mwa Gaza hii leo, ikiwa ni siku moja baada ya kuwauwa Wapalestina 274 wakati wa operesheni ya kuwaokoa mateka.

https://p.dw.com/p/4gqVn
Gaza | Kambi ya Nuseirat
Wapalestina wakiangalia uharibifu uliofanyika baada ya shambulio la bomu la Israel katika kambi ya wakimbizi ya Nuseirat, Ukanda wa Gaza, Jumamosi, Juni 8, 2024.Picha: Jehad Alshrafi/AP Photo/picture alliance

Wakaazi wa Hamas na vyombo vya habari vya Hamas wamesema vifaru vya Israel viliingia ndani kabisa ya Rafah katika jaribio la kutaka kuifunga kabisa sehemu ya mji huo wa kusini.

Katika taarifa mpya iliyotolewa leo na wizara ya afya ya Gaza inayodhibitiwa na Hamas, idadi ya Wapalestina waliouawa imefikia 274 kutoka 210 iliyoripotiwa jana, na wengine 698 wamejeruhiwa wakati makomando maalum wa Israel waliivamia kambi ya wakimbizi ya Al-Nuseirat kuwaokoa mateka wanne walioshikiliwa tangu Oktoba 7 na wanamgambo wa Hamas.

Soma pia: Israel yawaokoa mateka wanne wakiwa hai huko Gaza

Ofisi ya habari ya serikali ya Gaza imesema 64 ya waliouawa ni watoto na 57 ni wanawake.

Jeshi la Israel limesema kuwa askari wake aliuawa katika makabiliano ya risasi na wanamgambo waliokuwa wakitokea kwenye majengo ya makaazi.

Aidha limesema linafahamu kuwa chini ya Wapalestina 100 waliuawa, ijapokuwa halijasema ni wangapi kati yao walikuwa ni wapiganaji au raia.