1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yaapa kujibu shambulizi la Milima ya Golan

29 Julai 2024

Baraza la Usalama wa Taifa la Israel limeipatia idhini serikali ya Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu ya kuamua hatua za kuchukua kujibu shambulizi la roketi lililosababisha vifo vya vijana na watoto 12.

https://p.dw.com/p/4iqI2
Israel| Milima ya Golan| Lebanon
Athari za shambulizi kwenye kitongoji Majdal Shams kilichopo milima ya Golan.Picha: Hassan Shams/AP/picture alliance

Shambulizi hilo limetokea kwenye eneo linalokaliwa kwa mabavu na Israel la milima ya Golan.

Israel na Marekani zinalilaumu kundi la wanamgambo wa Lebanon la Hezbollah kuhusika na hujuma hiyo ya siku ya Jumamosi lakini kundi hilo limekanusha madai hayo.

Shambulizi hilo kwenye kitongoji cha Majdal Shams ndiyo mbaya zaidi kutokea ndani ya Israel au katika maeneo inayoyakalia tangu uvamizi wa kundi la Hamas wa Oktoba 7 mwaka jana, uliosababisha kuzuka kwa vita vya Gaza.

Israel iliapa kwamba itajibu shambulizi hilo dhidi ya Hezbollah na tayari jana Jumapili ndege za kivita za nchi hiyo ziliyapiga maeneo kadhaa ndani ya Lebanon.