1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIsrael

Israel yaanza kuwakusanya wanajeshi na polisi wa ziada

8 Aprili 2023

Israel imeanza kuwaita polisi na wanajeshi wa akiba baada ya mashambulizi yaliyosababisha vifo vya watu watatu, akiwemo mtalii mmoja raia wa Italia, yaliyofanywa huko Tel Aviv na Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kimabavu.

https://p.dw.com/p/4Ppxx
Israel | Machafuko mjini Jerusalem
Ghasia zimeongezeka tangu polisi wa Israel walipopambana na Wapalestina ndani ya eneo la msikiti wa Al-aqsa, mjini Jerusalem.Picha: AHMAD GHARABLI/AFP/Getty Images

Licha ya miito ya kutuliza mivutano, ghasia zimeongezeka tangu polisi wa Israel walipopambana na Wapalestina ndani ya eneo la msikiti wa Al-Aqsa katika mji unaozozaniwa wa Jerusalem siku ya Jumatano, pamoja na hatua ya Israel ya kuvurumisha makombora kuelekea Gaza na Lebanon, ikijibu mashambulizi ya awali ya maroketi yaliyofanywa na wanamgambo wa Palestina.

Raia huyo wa Italia aliuawa na watalii wengine saba walijeruhiwa katika shambulizi hilo la jana Ijumaa huko Tel Aviv kabla ya mshambuliaji, dereva taxi aliyetokea mji wa Kiarabu wa Kfar Kassem katikati ya Israel, kuuliwa na polisi, hii ikiwa ni kulingana na vikosi vya huduma za dharura na polisi. Waziri mkuu wa Italia Giorgia Meloni amemtaja mtalii huyo kuwa ni Alessandro Parini, 36 na tayari polisi ya Israel imeanzisha uchunguzi ya wahusika wa shambulizi hilo.

Kufuatia shambulizi hilo la Tel Aviv, waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amewaagiza polisi kuwaita polisi wote wa akiba kutoka vikosi mbalimbali na kulielekeza jeshi pia kuongeza vikosi vya ziada, hii ikiwa ni kulingana na ofisi yake.

Vikosi vya usalama vilipelekwa katika mji wa Huwara wa Ukingo wa Magharibi, Februari 26, 2023 kufuatia kifo cha Waisraeli wawili katika shambulio la risasi.
Ghasia zimeendelea kushuhudiwa katika eneo la Ukingo wa Magharibi na hata Ukanda wa Gaza kutokana na mashambulizi ya visasi.Picha: Ahmad Gharabli/AFP

Jeshi la polisi tayari limesema vikosi vinne vya akiba vya polisi wa mpakani vitapelekwa katikati mwa jiji kuanzia kesho Jumapili na kuungana na polisi ambao tayari walikuwepo mjini Jerusalem na mji wa Lod, katikati mwa taifa hilo ambao una mchanganyiko wa Wayahudi na Waarabu.

Vuguvugu la Kiislamu la Hamas la Palestina, linalodhibiti eneo la Gaza limelielezea shambulizi hilo kama "jibu la kawaida na halali" kwa Isreal kufuatia hatua yake ya kuuvamia msikiti wa Al-Aqsa. Mapema jana Ijumaa, ndugu wawili raia wa Uingereza na Israel waliuawa huku mama yao akijeruhiwa vibaya baada ya gari lao kulipuliwa na katika eneo la Bonde la Jordan lililoko Ukingo wa Magharibi.

Na taarifa kutoka Brussels, zimesema Umoja wa Ulaya umelaani mashambulizi hayo nchini Israel na kutoa wito wa pande zote kujizuia na kusitisha mashambulizi.

Soma Zaidi: Jamii ya kimataifa yalaani machafuko ya Al-Aqsa Jerusalem

Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja huo Josep Borrell kwenye taarifa yake aidha amekemea mashambulizi aliyoyaita ya "kiholela" ya maroketi yaliyorushwa kutokea Lebanon na Ukanda wa Gaza.

"Tunaziomba pande zote kujizuia, kuzuia kusambaa zaidi kwa machafuko na kuhamasisha utulivu katika kipindi hiki cha sikukuu za kidini," Borrell alisema na kuongeza kuwa "hadhi ya mahala patakatifu ni lazima ilindwe".

Soma Zaidi:Biden: Palestina tumieni siasa kupata amani ni Israel