1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rivlin ataka Abbas arudi kwenye mazungumzo

Mohammed Khelef19 Januari 2015

Israel imeanzisha kampeni ya kimataifa kuizuia ICC kuchunguza mashambulizi kwenye ardhi za Wapalestina, huku rais wa nchi hiyo akimtaka mwenzake wa Palestina kushiriki majadiliano.

https://p.dw.com/p/1EMVY
Waziri wa Mambo ya Nje wa Israel, Avigdor Lieberman, anayeongoza kampeni ya kimataifa dhidi ya ICC.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Israel, Avigdor Lieberman, anayeongoza kampeni ya kimataifa dhidi ya ICC.Picha: Reuters

Waziri wa Mambo ya Nje wa Israel, Avigdor Lieberman, alisema nchi yake inazishawishi nchi wanachama wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) kukata michango yake kwa mahakama hiyo, kama hatua yao dhidi ya uchuguzi wa awali wa ICC juu ya uwezekano wa kutendeka uhalifu wa kivita kwenye ardhi ya Wapalestina.

Akizungumza kabla ya mkutano wake wa Jumapili na mwenzake wa Canada, John Baird, Lieberman alisema ikiwa ICC haitobadilisha uamuzi wake wa kuanzisha uchunguzi huo, basi Israel itaelekeza hatua zake kwenye kuudhoofisha uwezo wa kifedha wa mahakama hiyo, ambayo huwa inaendeshwa kwa michango ya mataifa wanachama 122 kwa mujibu wa uwezo wa kiuchumi wa kila mwanachama.

"Tunadhani kwamba ni jambo lisilokubalika kwamba kundi la kigaidi kama Hamas litakuwa na uwezo wa kufungua kesi dhidi ya Israel hali sote tunakumbuka kuwa Hamas iliwatumia raia wake kama ngao.... Kama hakutakuwa na mabadiliko kwenye msimamo wa ICC, tutawaomba marafiki zetu kuacha kuichangia mahakama hiyo," alisema Lieberman.

Ujerumani, Japan kuombwa kuisusia ICC

Afisa mwengine wa Israel aliliambia shirika la habari la Reuters kwamba maombi ya kuikatia michango ya fedha mahakama ya ICC tayari yameshatumwa serikali za Ujerumani na pia yatawasilishwa kwa Waziri Mkuu wa Japan, Shinzo Abe, ambaye pia anaitembelea Israel na ambaye nchi yake ni mchangiaji mkubwa wa ICC.

Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu.
Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu.Picha: AFP/Getty Images/M. Alexandre

Naye Baird alirejelea msimamo wa serikali yake ya kihafidhina, ambayo daima imekuwa muungaji mkono mkubwa wa Israel, akisema kwamba Canada inaunga mkono haki ya Israel kujilinda na inapinga hatua ya Palestina kwenye ICC.

"Ninasisitiza msimamo wa Canada juu ya hatua ya Serikali ya Palestina kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu. Canada inasema kwa uwazi kabisa kwamba hatua hizi zilikuwa za uchokozi, za upande mmoja na haziwezi kuchangia kwenye amani na usalama katika eneo hili," alisema Baird.

Akiwa mjini Ramallah mapema hapo Jumapili, waziri huyo wa mambo ya nje wa Canada alijikuta kwenye kipindi kigumu sana baada ya waandamanaji kumtupia mayai-viza, wakimlaumu kwa mchango wa Canada kwa dola ya Israel.

Picha zilizorushwa na kituo cha televisheni cha Channel 2 cha Israel zilimuonesha Baird akishambuliwa kwa maneno na waandamanaji wa Kipalestina waliomuita "Bibi Baird". Bibi ni jina la utani la Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu.

Canada ilikuwa moja ya nchi tisa tu zilizopinga Palestina kutambuliwa kuwa mwanachama asiye na hadhi ya dola kwenye Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwaka 2012, ambapo mataifa mengine 138 yaliikubalia.

Rivlin amtaka Abbas wazungumze

Wakati hayo yakiendelea, Rais Reuven Rivlin wa Israel alimtaka mwenzake wa Palestina, Mahmoud Abbas, kurejea kwenye mazungumzo ya kusaka amani badala ya kutumia mahakama ya ICC au Umoja wa Mataifa.

Rais Reuven Rivlin wa Israel anamtaka Rais Mahmoud Abbas wa Palestina kurudi kwenye meza ya mazungumzo.
Rais Reuven Rivlin wa Israel anamtaka Rais Mahmoud Abbas wa Palestina kurudi kwenye meza ya mazungumzo.Picha: Reuters

Rivlin aliuambia ujumbe wa maseneta wa Marekani unaoitembelea sasa Israel ukiongozwa na Seneta John McCain kuwa kwa sasa hakuna njia nyengine ila majadiliano ya moja kwa moja.

"Namtolea wito Rais Abbas kwamba badala ya kwenda The Hague au Umoja wa Mataifa, njoo Jerusalem. Njoo uzungumze moja kwa moja na serikali na watu wa Israel," alisema Rais Rivlin.

Mapema mwezi huu, Palestina iliomba kuwa mwanachama wa mahakama hiyo ya ICC na Ijumaa iliyopita mahakama hiyo ikatangaza kuanzisha uchunguzi wa awali juu ya vitendo vya Israel kwenye mamlaka ya Palestina, vikiwemo vita vya mwaka 2014 dhidi ya Ukanda wa Gaza.

Mwandishi: Mohammed Khelef/Reuters/AFP
Mhariri: Josephat Charo