Israel imeahirisha ujenzi nyumba mpya za Waisrael
28 Desemba 2016Ijumaa iliyopita Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilitaka kusitishwa kwa sehemu ya mradi huo katika azimio lililowezeshwa na Marekani kujizuia kupiga kura. Miradi hiyo katika eneo ambalo Israel ililivamia mwaka 1967 katika vita vya Mashariki ya Kati na ambayo Wapalestina wanatafuta kuwa sehemu ya mji wao wa baadae, ni sehemu ya shughuli ambazo Umoja wa Mataifa ulitaka zisitishwe.
Katika hotuba yake, Waziri wa Mambo ya nje wa Marekani John Kerry, pamoja na mambo mengine anatarajiwa kuzungumzia hatua ya Marekani kujizuia kwenye kura yake ya turufu pamoja na kuelezea malengo juu ya azimio la kumalizika kwa mzozo kati ya Israel na Palestina.
Kukiwa na agenda za maombi ya vibali vya ujenzi vipatavyo 494 katika makaazi ya maeneo ya mijini katika eneo la Ramot na Ramot Shlomo, kamati ya wajumbe wa mipango na ujenzi katika mji wa Yerusalem imesema kuwa zoezi la kupiga kura kwa ajili ya kuidhinisha ujenzi wa nyumba hizo umefutwa kufuatia ombi la Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu.
Mwenyekiti wa jopo Meir Turgeman alisema katika kikao kuwa, Netanyahu amekuwa na mashaka kuhusu kuruhusu kufanyika kwa kura hiyo na kusema kuwa kungeweza kumpa Kerry kile alichokiita kitu cha kuzingatia kabla ya kutoa hotuba yake.
Msimamo wa Marekani katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa umevunja sera ya muda mrefu ya kidiplomasia ambayo ilikuwa ngao ya Israel iliyokuwa ikitumiwa na Marekani. Israel imelaani kitendo hicho na kusema kuwa ni kitendo cha aibu, na kinatazamwa kama kufunguliwa kwa risasi toka kwa Barack Obama dhidi ya Netanyahu na sera yake ya ujenzi wa makaazi.
Viongozi hao wawili wamekuwa na uhusiano mgumu, wakiwa wamegawanyishwa na sera ya Israel ambayo imedumu kwa miongo kadhaa ya ujenzi wa makaazi ya Wayahudi katika mipaka iliyochukuliwa pamoja na jinsi ya kuzuia silaha za nyuklia za Iran.
Marekani inautazama mradi wa ujenzi wa makaazi hayo kuwa ni kinyume cha sheria na mataifa mengi pia yanautazama kama kikwazo cha amani. Israel haikubaliani na hoja hiyo huku ikiinukuu Biblia, uhusiano wa kihistoria na kisiasa wa eneo hilo madai ambayo ni sawa na ya Palestina pamoja na maslahi ya kiusalama.
Mwandishi: Celina Mwakabwale/Reuters
Mhariri: Grace Patricia Kabogo