1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroIsrael

Israel yaadhimisha mwaka mmoja tangu shambulizi la Oktoba 7

7 Oktoba 2024

Israel inaadhimisha mwaka mmoja tangu mashambulizi ya Oktoba 7, 2023. Shambulio la Hamas kusini mwa Israel linachukuliwa kuwa shambulio baya zaidi dhidi ya Wayahudi tangu unyama wa enzi ya manazi.

https://p.dw.com/p/4lU0U
Waanfamanaji mjini Ottawa- Canada
Mmoja wa waandamanaji wanaounga mkono Israel akiwa ameshika bendera ya Israel wakati wa maandhimisho ya mwaka tangu Hamas ilipoishambulia Israel Oktoba 7, 2023Picha: picture alliance / ASSOCIATED PRESS

Rais wa Israel Isaac Herzog ameongoza maadhimisho ya kimataifa ya kumbukumbu ya mwaka wa kwanza wa shambulio hilo baya la Hamas la Oktoba 7 huku kumbukumbu zikifanyika kuwaenzi wahanga na mateka ambao bado wanashikiliwa katika Ukanda Gaza.

Herzog amesema "hili ni kovu dhidi ya ubinadamu. Hili ni kovu kwenye uso wa Dunia. Tunapaswa kufanya chochote tunachoweza kwa njia zote na zinazowezekana kuwarudisha mateka wetu."

Shambulio la Hamas lililoilenga jamii na watu waliokuwa kwenye tamasha la muziki kusini mwa Israel linachukuliwa kuwa shambulio baya zaidi dhidi ya Wayahudi tangu unyama wa enzi ya manazi.

Hapa nchini Ujerumani, wanaharakati walikusanyika katika lango la Brandenburg katikati mwa mji mkuu, Berlin Jumatatu asubuhi ambapo majina ya watu 1,170 waliouawa yalisomwa na pia majina ya wale 255 waliotekwa nyara. Mpaka sasa, karibu watu 100 bado wanashikiliwa mateka katika Ukanda wa Gaza na haijulikani ikiwa wako hai au wamekufa.

Maandamano pia yamefanyika katika nchi mbalimbali dunaini kupinga vita vya Gaza na nchini Lebanon vilivyosababishwa na shambulio la Oktoba 7 mwaka uliopita katika ardhi ya Israel.

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amesema jeshi la Israel "limebadilisha sura halisi" katika mwaka mmoja tangu mashambulizi ya Hamas na amesisitiza kuwa Israel itaibuka mshindi kutokana na kazi ya jeshi lake. Wakati huo huo, mashambulizi mapya yametikisa kusini mwa Beirut, ambayo inachukuliwa kuwa ngome ya Hezbollah.