1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel: Ujenzi wa makazi ya walowezi si kipaumbele kwa sasa

Yusra Buwayhid
22 Julai 2020

Waziri wa mambo ya nje wa Israel, Gabi Ashkenazi, amesema suala la ujenzi wa makazi ya walowezi wa Kiyahudi katika Ukingo wa Magharibi, halijapewa kipaumbele katika ajenda ya serikali kwa sasa.

https://p.dw.com/p/3fgep
Israel Jerusalem | Coronavirus | Benjamin Netanyahu
Picha: picture-alliance/dpa/G. Tibbon

Ashkenazi ametoa kauli hiyo kutokana na kwamba Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu alikuwa akitarajiwa kuanza mipango hiyo ya upanuzi wa makazi ya walowezi katika eneo linalokaliwa na Wapalestina kwenye Ukingo wa Magharibi mnamo Julai mosi. Lakini tarehe hiyo imepita na Netanyahu hakusikika akilizungumzia suala hilo.

“Hivi sasa kilicho muhimu zaidi ni usalama wa taifa la Israel,” amesema Ashkenazi, wakati akizungumza na gazeti la kila siku la Israel, Yediot Ahronot.

“Tunashikilia msimamo wetu, na mipango yetu ya upanuzi sio siri,” ameongeza. “Lakini hivi sasa tunajikita zaidi katika kuushughulikia uchumi ulioathirika pamoja na kupambana na janga la ugonjwa wa COVID-19. “

Israel Jerusalem | Proteste Coronavirus | Benjamin Netanyahu
Tunaandamana na pia tunajikinga na virusi vya coronaPicha: picture-alliance/dpa/D. Hill

Jumuiya ya Kimataifa imekuwa ikiipinga mipango hiyo ya ujenzi kwenye ardhi ya Wapalestina. 

Ujenzi huo wa Israel, unategemea kufuata mpango wa amani ya Mashariki ya Kati wa Rais wa Marekani Donald Trump kama muongozo, ambao umepingwa vikali na Wapalestina. 

Mpango huo uliopendekezwa na Marekani, umeipa Israel udhibiti wa asilimia 30 ya eneo la Ukingo wa Magharibi, ambalo limekuwa likikaliwa kwa nguvu na Israel tangu ilipolinyakuwa mwaka 1967. Asilimia 70 ya ardhi wataachiwa Wapalestina lakini litakuwa ni eneo lilogawika. 

Hata hivyo, haijulikani hakika Israel inapanga kunyakuwa kiasi gani cha eneo hilo. 

Wakati hayo yakijiri, waandamanaji wa Israel walikusanyika nje ya mlango wa kuingilia bungeni leo asubuhi, kufuatia maandamano ya usiku kucha ya kumpinga Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu. 

Polisi waliwakamata watu wanne na kuutawanya mkusanyiko huo, uliokuwa ukipinga kura inayotarajiwa kupigwa ili kuipa serikali mamlaka kamili bila ya kulishirikisha bunge katika kuchukua hatua za kupambana na janga la virusi vya corona. 

Maandamano hayo yanafanyika katika wakati ambapo baadhi ya raia wa Israel wamekuwa wakionyesha hali ya kutoridhishwa na uongozi wa Netanyahu.

Israel: Wohnungsbau in Ostjerusalem
Ujenzi wa makazi ya walowezi mashariki mwa JerusalemPicha: picture-alliance/N. Alon

Awali Israel ilisifiwa kwa kuchukua hatua za haraka za kupambanana janga la virusi vya corona. Lakini tangu vikwazo kulegezwa manmo mwezi Mei, maambukizi mapya yamekuwa yakijitokeza. Kiwango cha ukosefu wa ajira pia kimeongezeka kwa asilimia 3.9 tangu kabla ya kuanza janga hilo.

Wakosoaji wanasema serikali ya Netanyahu haikutoa msaada wa kutosha kwa raia katika kukabilianana mgogoro wa kiuchumi uliotokana na maambukizi ya virusi vya corona. Aidha wakosoaji hao wanasema serikali ilishindwa kuwasaidia wafanyabiashara nchini humo wakati huu wenye ugumu wa kiuchumi.