Israel kupunguza wanajeshi wake kutoka Ukanda wa Gaza
1 Januari 2024Katika taarifa hii leo, jeshi hilo la Israel, limesema maelfu ya wanajeshi wake wataondolewa kutoka Gaza katika muda wa wiki zijazo kwa mafunzo na mapumziko.
Hatua ya jeshi hilo inaweza kuashiria kuwa mapigano yanapunguzwa katika baadhi ya maeneo ya Gaza,hasa katika nusu ya eneo la Kaskazini ambapo jeshi hilo linasema linakaribia kuchukua udhibiti.
Israel imekuwa chini ya shinikizo la Marekani
Israel imekuwa ikishinikizwa na mshirika wake mkuu, Marekani, kuanza kupunguza makali ya vita hivyo, ambavyo wizara ya afya ya Gaza inasema vimeshaangamiza maisha ya watu wapatao 22,000.
Soma pia:Jeshi la Israel ladai kuharibu maficho ya wanamgambo wa Hamas huko Gaza
Maelezo kuhusu kupunguzwa kwa wanajeshi hao yanakuja kabla ya ziara ya waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken katika eneo hilo na baada ya utawala wa Biden kutolihusisha bunge kwa mara ya pili mwezi huu kuidhinisha uuzaji wa dharura wa silaha kwa Israel.