1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel kupunguza operesheni zake za kijeshi Gaza

16 Januari 2024

Israel imesema imeanza kupunguza operesheni zake za kijeshi dhidi ya kundi la Hamas kusini mwa Gaza, baada ya wizara ya afya iliyo chini ya kundi hilo la wanamgambo kusema kuwa idadi ya watu waliouawa imezidi 24,000.

https://p.dw.com/p/4bIx2
Vikosi vya Israel vikiwa katika Ukanda wa Gaza
Vikosi vya Israel vikiwa katika eneo la kusini mwa Ukanda wa GazaPicha: Ohad Zwigenberg/AP/picture alliance

Waziri wa Ulinzi wa Israel, Yoav Gallant amesema operesheni kubwa ya kijeshi dhidi ya wanamgambo wa Hamas itamalizika hivi karibuni. Katika wiki za hivi karibuni jeshi la Israel lilizidisha operesheni zake kwenye miji ya kusini ya Khan Younis na Rafah, baada ya kubainisha kuwa miundo ya kijeshi ya Hamas kwenye eneo la kaskazini imeharibiwa.

Gallant amewaambia waandishi habari kuwa Israel iliweka wazi kwamba operesheni ya kijeshi ingedumu kwa takribani miezi mitatu, na kwamba hatua hiyo tayari inafanikiwa kaskazini mwa Ukanda wa Gaza. Amesema kusini mwa Gaza kampeni ya kijeshi itamalizika hivi karibuni, na kwenye maeneo yote mawili, utafika wakati ambapo watahamia katika awamu inayofuata, bila ya kutoa ufafanuzi zaidi.

Ikiwa ni zaidi ya siku 100 tangu kuanza kwa vita kati ya Israel na wapiganaji wa Hamas, serikali ya Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu imekabiliwa na shinikizo la kimataifa, likimtaka avimalize vit hivyo, wakati ambapo vifo vya raia vinaongezeka na mzozo wa kibinadamu huko Gaza unazidi kuwa mbaya.

Umoja wa Mataifa wataka vita visitishwe

Waziri wa Ulinzi wa Israel, Yoav Gallant
Waziri wa Ulinzi wa Israel, Yoav GallantPicha: Ariel Hermoni/Israel Mod/IMAGO

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres jana Jumatatu alirudia na kusisitiza wito wa kusitishwa kwa mapigano hayo, ili kuhakikisha msaada wa kibinaadamu unafika pale inapohitajika, pamoja na kuratibu mpango wa kuachiliwa kwa wafungwa, kwa sababu kadri mzozo huo unavyoendelea, ndivyo hatari inavyoongezeka.

''Hali ya kibinadamu huko Gaza haielezeki. Hakuna mahali ambako ni salama na hakuna mtu aliye salama. Ingawa pamekuwa na baadhi ya hatua za kuratibu msaada wa kiutu kuongezeka Gaza, huduma za kuokoa maisha ya watu hazipatikani kwa watu ambao wanahitaji. Ninasikitishwa sana na ukiukwaji wa wazi wa sheria ya kimataifa ya kibinadamu ambayo tunashuhudia," alifafanua Guterres.

Makumi ya watu wauawa Gaza

Wakati huo huo, ghasia katika eneo la Ukingo wa Magharibi linalokaliwa kimabavu na Israel, ufyatulianaji wa risasi katika mpaka wa Israel na Lebanon, na mashambulizi ya vikosi vya Marekani dhidi ya waasi wa Yemen wanaoungwa mkono na Iran wanaoonyesha mshikamano na Hamas, yote yameibua hofu ya vita hivyo kuongezeka zaidi na kuvuka zaidi ya Ukanda wa Gaza. Marekani, Umoja wa Ulaya, Ujerumani na mataifa mengine kadhaa ya Magharibi yameiorodhesha Hamas kuwa kundi la kigaidi.

Israel yaendeleza mashambulizi Gaza

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio GuterresPicha: Shannon Stapleton/REUTERS

Hayo yanajiri wakati ambapo jeshi la Israel limesema kuwa wanajeshi wake wamewaua wanamgambo kadhaa wa Kipalestina, karibu na mji wa Bei Lahia ulioko kaskazini mwa Gaza. Jeshi hilo limesema pia wakati wa operesheni ya jeshi la IDF kwenye eneo hilo, wanajeshi walipata takribani mitambo 100 ya kurushia roketi na makombora 60 ambayo yalikuwa tayari kwa ajili ya kutumika.

Umoja wa Mataifa: Hali Ukanda wa Gaza inatisha

Jeshi hilo pia limesema vikosi vyake maalum vimefanya mashambulizi kwenye eneo la Ayta ash Shab nchini Lebanon, kwa lengo la kuondoa kitisho kilichowekwa katika eneo hilo. Hata hivyo, jeshi hilo halikufafanua zaidi ni vikosi vipi ambavyo vimefanya mashambulizi hayo, ingawa limesema ndege zake za kivita zimeshambulia mifumo ya kujilinda na makombora kusini mwa Lebanon.

(AFP, AP, Reuters)