1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel inawatesa Waeritrea na Wasudan

9 Septemba 2014

Ripoti mpya ya Human Rights Watch inasema serikali ya Israel imewalazimisha takribani raia 7,000 wa Sudan na Eritrea kurejea nyumbani katika nchi zao ambako wanakabiliwa na kitisho cha unyanyasaji.

https://p.dw.com/p/1D98C
Flüchtlingslager Holot für afrikanische Asylsuchende in Israel
Picha: Getty Images

Ripoti hiyo inasema baadhi ya Wasudan na Waeritrea waliorudi makwao wameteswa, kuwekwa kizuizini kiholela na kufunguliwa mashtaka ya uhaini kwa kukanyaga nchini Israel.

Ripoti hiyo inaelezea kwa kina namna ambavyo Israel ilivyokiuka sheria katika kuzuia juhudi za Waeritrea na Wasudan wanaotafuta hifadhi chini ya sheria za Israel na za kimataifa. Maafisa wa Israel wanawataja raia wa Eritrea na Sudan kuwa ni kitisho kwa usalama wa nchi na kuwanyima fursa ya kupata huduma za kuzingatia mchakato wa kutafuta hifadhi.

Flüchtlingslager Holot für afrikanische Asylsuchende in Israel
Kundi la watafutaji hifadhi likipelekwa katika kambi ya Holot nchini Israel chini ya ulinziPicha: Getty Images

Mtafiti mkuu wa masuala ya wakimbizi katika shirika hilo Gerry Simpson anasema hatua ya Israel kuyauwa matumaini ya watu kupewa hifadhi kwa kuwaweka katika mazingira magumu na kisha kudai kuwa wanaondoka nchini humo kwa hiari ni ukiukaji mkubwa wa haki zao.

Mnamo mwaka wa 2006, idadi kubwa ya Waeritrea na Wasudan walianza kuwasili Israel kupitia Rasi ya Sinai nchini Misri, wakikimbia vitendo vya ukiukaji wa haki za binaadamu katika nchi zao. Wakati Israel ilifunga mipaka yake mnamo Desemba 2012, karibu Waeritrea 37,000 na Wasudan 14,000 walikuwa wameingia nchini humo.

Tangu mwaka wa 2012, maafisa wa Israel wamewazuia maelfu ya Waeritrea na Wasudan wanaoingia nchini humo bila vibali maalum. Baada ya Mahakama ya Juu Kabisa ya Israel kuamuru mwezi Septemba 2013 kuwa hatua ya kuwazuia watu kiholea ilikuwa kinyume cha sheria, serikali ya Israel ilijibu kwa kuipa jina jipya sera yake ya kuwazuilia watu. Hapo ndipo ilianza kuwakamata na kuwapeleka katika Kituo cha Makazi cha Holot kilichoko katika jangwa la Negev.

Asylsuchende protestieren gegen israelische Regierung
Kumekuwa na maandamano nchini Israel yanayyofanywa na watu wanaotafuta hifadhiPicha: picture-alliance/dpa

Kufikia mwishoni mwa Agosti mwaka huu, ni chini ya Waeritrea na Wasudan 2,000 pekee ikiwa ni pamoja na 1,000 waliodai kupewa hifadhi walizuiliwa katika kambi ya Holot huku wengine chini ya 1,000 wakizuiliwa katika kituo cha Saharonim. Wanaobaki 41,000 katika miji ya Israel wanaishi chini ya kitisho cha kuwataka waende katika kambi ya Holot.

Mnamo Februari 2013, Israel iliwaruhusu raia hao kuwasilisha maombi ya kupewa hifadhi. Lakini kufikia Machi 2014, ni maombi 450 pekee yaliyokuwa yamezingatiwa. Chini ya sheria za Sudan, yeyote anayezuru Israel anakabiliwa na hadi kipindi cha miaka 10 jela nchini Sudan.

Human Rights Watch imeitaka serikali ya Israel kuwatambua raia wa Sudan na Eritrea wanaoishi nchini humo kama wakimbizi kwa mujibu wa mwongozo wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuwashughulikia Wakimbizi. Kutokana na vitendo vya ukiukaji wa haki za binaadamu katika nchi zao, serikali ya Israel inapaswa kuwapa Waeritrea na Wasudan hadi ya kibali cha muda cha ulinzi kwa kinachoweza kutolewa upya mara baada ya musda wa miezi 12 unapomalizika, limesema shirika hilo, na kuongeza kuwa baada ya hapo raia hao wanaweza kuruhusiwa kurejea katika nchi zao kwa njia ya usalama na heshima, punde mazingira yatakapoimarika nyumbani.

Mwandishi: Bruce Amani/HRW
Mhariri: Gakuba Daniel