1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mpango wa kusitishwa mapigano Gaza unatarajiwa kuanza leo

Admin.WagnerD23 Novemba 2023

Mpango wa kusitishwa mapigano kwa siku nne kati ya Israel na Hamas ili kuruhusu msaada kuingia Gaza na kuwachiwa huru mateka wanaoshikiliwa unatarajiwa kuanza kutekelezwa kwa mara ya kwanza.

https://p.dw.com/p/4ZLAB
Nahostkonflikt - Gaza
Picha: Victor R. Caivano/AP/dpa/picture alliance

Hatua hiyo ni baada ya karibu wiki saba za vita.Hamas walisema mpango huo utaanza leo Alhamisi saa nne kamili asubuhi. Lakini Israel imesema mpango huo hautaanza hadi pengine kesho Ijumaa. Mshauri wa usalama wa taifa Tzachi Hanegbi amesema mawasiliano kuhusu kuwachiwa kwa mateka wao yanaendelea kupiga hatua.Wakizungumza mjini Tel Aviv jana usiku katika kikao cha pamoja cha waandishi habari Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu, waziri Benny Gantz na Waziri wa Ulinzi Yoav Gallant, wameapa kuwaleta nyumbani mateka wote na kuwaangamiza wanamgambo wa Hamas. Netanyahu amesema kuwa vita hivyo vitaendelea hadi watakapoyatimiza malengo yao. Chini ya mpango huo, mateka 100 wataachiwa kutoka Gaza kwa kubadilishana na wafungwa 300 wa Kipalestina wanaoshikiliwa nchini Israel. Aidha, malori yaliyobeba misaada ya dharura yataruhusiwa kuingia Ukanda wa Gaza ambako hakuna chakula, maji, umeme na dawa na vifaa vya matibabu.