1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Islamabad. Majeshi ya NATO yakataa ombi la kupeleka helikopta kuwaokoa watu walionaswa katika maeneo ya milima.

22 Oktoba 2005
https://p.dw.com/p/CEPZ

Majeshi ya NATO yamekataa ombi la dharura la umoja wa mataifa la kuanza kuwaondoa watu kwa wingi kwa ndege ili kuwaokoa mamia kwa maelfu ya wahanga wa tetemeko la ardhi waliokwama katika maeneo ya milima ya Himalaya kabla ya majira ya baridi kali kuanza.

Usafiri wa Helikopta ndio njia pekee ya kuweza kufikia katika maeneo ya ndani ya milimani katika jimbo la Kashmir nchini Pakistan katika mpaka wake wa kaskazini magharibi.

Badala yake NATO imekubali kutuma wanajeshi wake 1,000 kuwasaidia watu walionusurika ambao wamekuwa wakingojea msaada kwa muda wa wiki mbili sasa.

Kamishna wa umoja wa mataifa anayeshughulikia wakimbizi Bwana Antonio Guterres , amesema kuwa wakati ni huu kwa jumuiya ya mataifa kuweza kutekeleza majukumu yake. Tetemeko la ardhi lililotokea Oktoba 8 limesababisha vifo vya watu zaidi ya 50,000 na idadi hiyo bado inatarajiwa kuwa itaendelea kuongezeka.