1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

IS yauwa wanajeshi 32 wa Libya

19 Mei 2016

Wanajeshi 32 watiifu kwa serikali ya Libya wameuawa katika makabiliano na kundi la IS na katika mashambulizi ya kujitoa mhanga. Hayo yamethibitishwa na jeshi la nchi hiyo ambalo pia limesema watu wengine 50 wamejeruhiwa.

https://p.dw.com/p/1IqKs
Wanajeshi wa Libya wameripotiwa kusonga mbele kuelekea ngome ya Dola la Kiislamu-IS.
Wanajeshi wa Libya wameripotiwa kusonga mbele kuelekea ngome ya Dola la Kiislamu-IS.Picha: picture-alliance/Photoshot/Hamza Turkia

Serikali hiyo ya Libya inayotambuliwa na Umoja wa Mataifa imesema vikosi vyake vilikuwa vikisonga mbele kuelekea mji wa Sirte, ambao ni ngome kuu ya kundi la IS nchini Libya, na kwamba wapiganaji wake waliweza kuikomboa miji mitatu iliyokuwa imetekwa na IS mwanzoni mwa mwezi huu.

Katika mapambano yaliyotokea serikali imewapoteza wapiganaji wake 32, wakiwemo 20 waliouawa katika mripuko wa gari uliosababishwa na mshambuliaji wa kujitoa mhanga kwenye kituo cha ukaguzi wa barabarani cha al-Khamees, kilichoko umbali wa km 50 kutoka mji wa Sirte.

Duru za hospitali ya Misrata, eneo lenye nguvu kubwa kijeshi ambalo linaegemea upande wa serikali ya Umoja wa Kitaifa, zimethibitisha kutokea kwa mashambulizi hayo ya kujitoa mhanga, na idadi ya wanajeshi 20 waliouawa.

IS yakiri kuhusika

Katika taarifa iliyosambazwa kupitia mitandao ya kijamii, wafuasi wa Dola la Kiislamu wamedai kuhusika na shambulizi hilo, lakini shirika la habari la DPA halikuweza kuthibitisha madai yao hayo.

Libya imetumbukia katika ghasia tangu kuangushwa kwa serikali ya Kanal Moamer Gaddafi mwaka 2011.
Libya imetumbukia katika ghasia tangu kuangushwa kwa serikali ya Kanal Moamer Gaddafi mwaka 2011.Picha: picture-alliance/dpa

Majina ya watu wawili waliotajwa na kundi hilo kufanya mashambulizi ya kujitoa mhanga dhidi ya vikosi vya serikali, yanaashiria kuwa mmoja alikuwa kutoka Sudan, na mwingine kutoka nchi ambayo siyo ya kiislamu.

Miji iliyokombolewa imetajwa kuwa Abugrein, al-Washka na Wadi Zamzam. Shirika la habari la Libya limenukuu vyanzo vya jeshi la serikali, vilivyosema mapigano ya kuikomboa miji hiyo yalijumusha pia wanamgambo wanaoiunga mkono serikali, na operesheni kutoka angani.

Afisa mmoja katika mji wa Abugrein Mohammed al-Jali ameiambia tovuti ya al-Wasat kwamba mashambulizi ya vikosi vitiifu kwa serikali yalikuwa ya kushitukiza, na yaliwalazimisha wapiganaji wa IS kuzikimbia ngome zao, wakiacha nyuma maiti nyingi za wenzao.

Kanali miongoni mwa waliouawa

Ripoti moja imesema katika mapigano ya Jumanne wanajeshi wa serikali wasiopungua sita waliuawa, akiwemo afisa mmoja mwenye cheo cha kanali. Wapiganaji wengine 15 walijeruhiwa katika mapigano hayo, kwa mujibu wa ripoti hiyo.

Kundi la IS limejiimarisha katika mji wa Sirte na maeneo yanayouzunguka.
Kundi la IS limejiimarisha katika mji wa Sirte na maeneo yanayouzunguka.Picha: Reuters/G. Tomasevic

Libya imetumbukia katika mgogoro wa kivita tangu mwaka 2011, kufuatia vuguvugu la uasi lililomtimua madarakani Muamar Gaddafi, aliyeiongoza kiimla nchi hiyo kwa muda mrefu.

Tangu mwaka 2014, Libya imegawika katika sehemu mbili kuu kiutawala, moja inayotambuliwa kimataifa ikiwa na makao yakew katika mji wa mashariki wa Tobruk, na nyingine yenye mrengo wa kiislamu ikiudhibiti mji mkuu, Tripoli.

Kundi la IS limenufaika na hali hiyo ya misukosuko, kujiimarisha katika nchi hiyo yenye utajiri mkubwa wa mafuta. Kundi hilo lililochipuka kutoka kwenye mtandao wa al-Qaida limeweka ngome zake katika mji wa Sirte kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa, na zipo taarifa zinazosema limekuwa likiwahamisha maafisa wake na wapiganaji kutoka maeneo yake ndani ya Iraq na Syria, na kuwapeleka Sirte.

Mwandishi: Daniel Gakuba/dpae/afpe

Mhariri:Iddi Ssessanga