1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

IS yauwa 21 katika shambulizi la gereza Afghanistan

3 Agosti 2020

Shambulizi la kundi linalojiita Dola la Kiislamu – IS kwenye gereza moja la mashariki mwa Afghanistan linalowahifadhi mamia ya wafuasi wa kundi hilo limeendelea leo

https://p.dw.com/p/3gJzQ
Afghanistan Dschalalabad | Angriff auf Gefängnis | Nationale Sicherheitskräfte
Picha: Reuters/Parwiz

Afisa mmoja wa eneo hilo amesema watu wengine 43 wamejeruhiwa katika shambulizi hilo ambalo lilianza jana usiku wakati mlipuaji wa kujitoa muhanga wa IS alipoligongesha gari lake lilojaa mabomu kwenye lango kuu la gereza la Jalalabad.

Wapiganaji kisha wakaanza kufyatua risasi dhidi ya vikosi vya usalama katika jela hiyo ya makao makuu ya mkoa wa Nangarhar, karibu kilometa 115 kutoka mji mkuu wa Afghanistan Kabul.

Mpaka sasa washambuliaji watatu wameuawa lakini mapambano yaliendelea mapema leo huku milio ya risasi ikisikika kutoka kwenye gereza hilo. Msemaji wa gavana wa mkoa wa Nangarhar Attaullah Khogyani amesema waliouawa ni pamoja na raia, wafungwa, walinzi na vikosi vya usalama vya Afghanistan.

Soma pia: Afghanistan yasema haitawaachia huru wafungwa "hatari" wa Taliban

Polisi wanaamini wanamgambo kadhaa walikimbilia katika eneo moja la makaazi na kufanya iwe vigumu kupambana nao.

Tawi la IS nchini Afghanistan linalofahamika kama IS katika mkoa wa Khorasan, limedai kuhusika na shambulizi hilo. Makao yake makuu yako mkoani Nangarhar.

Kiini cha shambulizi hilo hakijabainika

Chanzo cha mapigano hayo yaliyoanza Jumapili usiku hakijabainika haraka
Chanzo cha mapigano hayo yaliyoanza Jumapili usiku hakijabainika harakaPicha: Reuters/Parwiz

Kiini cha shambulizi hilo hakijabainika haraka. Hata hivyo, baadhi ya mahabusu walitoroka wakati wa mapigano, kwa mujibu wa afisa mmoja wa mkoa ambaye hakutaka jina lake litajwe kwa sababu hana mamlaka ya kuzungumza na wanahabari.

Gereza hilo linawahifadhi karibu wafungwa 1,500, ambao mamia kadhaa wanaaminika kuwa wanachama wa IS.

Shambulizi hilo linakuja siku moja baada ya maafisa kusema vikosi maalum vya Afghanistan vilimuua kamanda mmoja mwandamizi wa IS karibu na Jalalabad.

Msemaji wa kisiasa wa Taliban Suhail Shaheen, aliliambia shirika la habari la AP kuwa kundi lake halikuhusika na shambulizi la Jalalabad. Marekani ilifikia makubaliano ya amani na Taliban mwezi Februari. Duru ya pili, na ambayo ni muhimu ya mazungumzo kati ya Taliban na uongozi wa kisiasa mjini Kabul haijaanza. Marekani na Jumuiya ya Kujihami ya NATO wameshaanza kuwaondoa wanajeshi nchini humo kama sehemu ya masharti ya muafaka huo.

Taliban ilitangaza siku tatu za kuweka chini silaha kuanzia Ijumaa kwa ajili ya siku kuu ya Eid al-Adha. Mpango huo ulikamilika usiku wa manane jana.