IS yakubaliana na kiapo cha utiifu cha Boko Haram
13 Machi 2015Akizungumza kupitia mkanda wa video, kwa niaba ya kiongozi wa kundi lenye itikadi kali linalojiita Dola la Kiislamu-IS, Abu Bakr al-Baghdadi, msemaji wa kundi hilo, Abu Mohammed al-Adnani, amesema wamekubaliana kuhusu kiapo cha utii kutoka kwa ndugu zao. Amesema wanawapongeza ndugu zao Waislamu na wapiganaji wa jihadi Afrika Magharibi na wamewataka Waislamu wote ambao hawawezi kupambana nchini Iraq na Syria, wapigane Afrika.
''Leo ninawatangazia kuongezeka kwa Ukhalifa hadi Afrika Magharibi. Khalifa, Mwenyezi Mungu amlinde, amekubali kiapo cha utiifu kutoka kwa kaka zetu wa Kisuni waliokubali wito wa kuwa wapiganaji wa Jihadi. Tunawapongeza kwa kumfata Khalifa wa Waislamu,'' alisema al-Adnani.
Siku ya Jumamosi kiongozi wa Boko Haram, Abubakar Shekau, alitangaza kulitii kundi la Dola la Kiislamu. Kwa mujibu wa msemaji huyo, hizo ni habari njema kwani lengo lililopo sasa ni kuanzisha Ukhalifa katika mataifa yote ya Afrika Magharibi. Adnani amesema ahadi ya utii iliyotolewa na Boko Haram imefungua mlango kwa ndugu zao Waislamu kuingia kwenye nchi ya Kiislamu na kuanza mapambano.
Tangazo la IS limetolewa wakati ambapo kundi hilo linapambana na majeshi ya Iraq katika mji wa Tikrit, huku nayo majeshi yanayoongozwa na Marekani yakifanya mashambulizi ya anga katika maeneo mengine ya nchi hiyo pamoja na Syria.
Afrika yaomba msaada wa Umoja wa Mataifa
Wakati huo huo, mataifa ya Afrika yameutaka Umoja wa Mataifa kuanzisha mfuko wa fedha kwa ajili ya kikosi cha kupambana na Boko Haram nchini Nigeria. Aidha, kulingana na rasimu ya azimio la Umoja wa Mataifa, jana (12.03.2015) wajumbe wa Baraza la Usalama la umoja huo, waliitaka jumuiya ya kimataifa kukisaidia kikosi cha jeshi kinachoyajumuisha mataifa matano ya Afrika kwa kuwapatia fedha, vifaa na msaada wa kijasusi.
Azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linaunga mkono kuanzishwa kwa kikosi cha Nigeria na nchi jirani za Cameroon, Chad, Niger na Benin ili kupambana na Boko Haram. Umoja wa Afrika tayari umeshaidhinisha kikosi chenye hadi wanajeshi 10,000.
Kundi la Boko Haram limesababisha mauaji ya zaidi ya watu 13,000 tangu lilipoanzisha mashambulizi mwaka 2009 kaskazini mwa Nigeria, katika harakati za kuanzisha taifa la Kiislamu litakalozingatia sheria ya Kiislamu ya Sharia.
Hata hivyo, kundi hilo liliongeza mashambulizi na kuvuka mipaka hadi Cameroon, Chad na Niger. Mashambulizi ya hivi karibuni yanayofanywa na majeshi ya nchi nne za Afrika yanaonekana kuyatwaa tena majimbo yaliyokuwa yanadhibitwa na waasi hao.
Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/APE,RTRE,AFPE
Mhariri:Josephat Charo