IS wafurushwa Kobane na wapiganaji wa kikurdi
27 Januari 2015Kukombolewa kwa mji wa Kobane kunakuja wakati wanamgambo wa IS wakipata pigo jingine nchini Iraq baada ya afisa wa ngazi ya juu wa jeshi nchini Iraq kusema wanajeshi wamefanikiwa kulikomboa jimbo la Diyala kutoka mikononi mwa IS.
Baada ya mapigano ya miezi minne katika mji wa mpakani kati ya Syria na Uturuki yaliyosababisha vifo vya zaidi ya watu 1,800,wapiganaji wa kikosi cha kijeshi cha kikurdi YPG wameweza kuwafurusha wapiganaji wa IS kutoka Kobane na kuudhibiti kikamilifu mji huo, hayo ni kulingana na shirika la kutetea haki za binadamu nchini Syria.
Wanamgambo waliosalia wanasakwa
Mkurugenzi wa shirika hilo Rami Abdel Rahman amesema wakurdi wanawaandama wanamgambo kadhaa viungani mwa mji wa Kobane upande wa mashariki lakini hakuna mapigano zaidi ndani ya mji wa Kobane.
Kituo kikuu cha jeshi la Marekani kimesema vikosi vya kikurdi kwa hivi sasa vinadhibiti asilimia tisini ya mji huo.Taarifa kutoka Marekani imesema licha ya kuwa vita dhdi ya IS havijakamilika, kushindwa kwa wanamgambo mjini Kobane kumewanyima mojawapo ya malengo yao makuu ya uasi.
Msemaji wa kikosi cha YPG Polat Jan ameandika katika ukurasa wa Twitter kusifu juhudi za wapiganaji wa kikurdi kuukomboa mji na watu wa Kobane.
Kwa hivi sasa wapiganaji hao wanafanya operesheni ya kuwasaka wanamgambo wachache waliosalia katika eneo la Maqtala na wanalikaribia eneo hilo kwa uangalifu kutokana na kitisho cha kuwa na mabomu ya kutegwa ardhini na kwenye magari.
Ushindi huo wa wakurudi unakuja baada ya wizara ya ulinzi ya Marekani kusema nchi hiyo na washirika wake wamefanya mashambulizi 17 ya angani dhidi ya wanamgambo wa IS katika maeneo kadhaa mjini Kobane katika kipindi cha saa ishirini na nne zilizopita.
Kukombolewa kwa Kobane ni pigo kwa IS
Mbali na kushindwa katika mji wa Kobane unaojulikana pia Ain al Arab, IS imewapoteza wapiganaji wake 1,196 tangu iuvamie mji huo tarehe 16 mwezi Septemba mwaka jana huku wakurdi wakiwapoteza wapiganaji 324.
Wachambuzi wanasema IS kuupoteza mji wa Kobane licha ya kuwa na silaha nyingi nzito ilizozipora kutoka kwa kambi za kijeshi, ni pigo kubwa kimkakati kwani walitumai kuuteka kikamilifu ili kulidhibiti eneo zima la mpakani kati ya Syria na Uturuki.
Tangu kundi hilo la IS kuanzisha uasi mwaka 2013, limeyateka maeneo makubwa nchini Syria na Iraq na kutangaza dola la kiislamu katika maeneo inayoyadhibiti huku ikifanya ukatili mkubwa ukiwemo kuwatesa na kuwachinja mateka wao.
Ushindi huo wa wakurdi wa Syria umewezeshwa na kampeini kabambe ya kijeshi kutoka kwa Marekani na washirika wake pamoja na kupigwa jeki na wapiganaji wa kikurdi wa kikosi cha Peshmerga kutoka Iraq walioingia mjini Kobane mwishoni mwa mwaka jana wakiwa na silaha nzito kuwasaidia wenzao kupambana na IS.
Mwandishi:Caro Robi/AFP/Dpa
Mhariri: Iddi Ssessanga