Iraq yatoa fedha kwa wakimbizi
19 Aprili 2007Serikali ya Iraq sasa inataka kuzisaidia nchi hizo katika kubadiliana na idadi kubwa ya wakimbizi. Hilo ndilo tokeo moja la mkutano wa shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia suala la wakimbizi uliofanyika Geneva, Uswisi.
Kwa mujibu wa kamishna wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia masuala ya wakimbizi, Antonio Guterres, serikali ya Irak iko tayari kuchukua jukumu la kuboresha hali ya wakimbizi wa Iraq wakiwa ndani au nje ya Iraq. Imeahidi kutoa Dola Millioni 25 kwa nchi za nje ili kuhakikisha huduma za afya. Serikali za Jordan na Syria hasa zilitaka kusaidiwa kifedha. Syria imechukua wakimbizi takriban millioni 1.2. Nchini Jordan wanaishi wakimbizi 750.000 wa kutoka Iraq. Antonio Guterres alitoa shukrani kwa nchi hizo na alisema huenda itabidi kufanywa mkutano wa kuchangisha fedha zaidi kwa wakimbizi wa Iraq baadaye mwaka huu.
Hadi sasa, sehemu kubwa ya Dola Millioni 60 zilizotakiwa kuwasaidia wakimbizi hawa zimeshaahidiwa na jamii ya kimataifa, alisisitiza Guterres. Tatizo kubwa zaidi lakini ni hali ya kivita inayoendelea nchini Iraq. Antonio Guterres: “Linalohitajika sasa ni suluhisho la kisiasa ambalo linamaliza mapigano ya kidini na kuleta maridhiano ya kitaifa. Hivyo tu wale watu ambao walitishiwa wataweza kurudi makwao na kuishi salama nchini Iraq.”
Mkutano wa Geneva ulioendelea kwa siku mbili ulihudhuriwa na wajumbe 450 kutoka nchi 60 pamoja na mashirika mengi ya kutoa misaada. Nchi kadhaa kama vile Ujerumani na Marekani zilitoa ahadi ya kuchangia fedha kuwasaidia wakimbizi, alisema kamishna Guterres wa Umoja wa Mataifa. Bw. Guterres pia aliarifu kuwa shirika lake la Umoja wa Mataifa linapanga kumtuma mwakilishi maalum kwa ajili ya Iraq hivi karibuni. Baada ya kushambuliwa makao makuu ya Umoja wa Mataifa nchini Iraq miaka minne iliyopita, mwakilishi huyu aliondoshwa kutoka Iraq.
Mawaziri wa ndani wa nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya wanatajariwa kukutana kesho kuzungumzia suala la wakimbizi wa Iraq. Kulingana na makadirio ya Umoja wa Mataifa, Wairaqi 20.000 wamekimbilia nchi za Umoja wa Ulaya. Mashirika yanayotetea haki za binadamu yalizitaka nchi za Umoja huo zichukue wakimbizi zaidi na kuacha kuwarejesha nyumbani wale walio nao. Wakati huo huo, Marekani imearifu itachukua wakimbizi zaidi ya elfu kumi kwa muda fulani.