1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iraq yadai kuwashinda ISIL Baiji

25 Juni 2014

Iraq inadai vikosi vyake sasa vinaudhibiti mtambo wa mafuta wa Baiji huku jumuiya ya kimataifa ikizidi kuishinikiza kuwajumuisha Wairaqi wote kuiunganisha dhidi ya misingi ya kimadhehebu na itikadi.

https://p.dw.com/p/1CPmO
Jeshi la Iraq likijitayarisha kuelekea uwanja wa mapambano katika mtambo wa mafuta wa Baiji.
Jeshi la Iraq likijitayarisha kuelekea uwanja wa mapambano katika mtambo wa mafuta wa Baiji.Picha: picture-alliance/dpa

Televisheni inayomilikiwa na serikali ya Iraq imeripoti kwamba mtambo huo mkubwa kabisa umetwaliwa na wanajeshi wa serikali baada ya mapambano makali na waasi. Hadi alfajiri ya Jumatano, kikosi maalum cha wapiganaji kutoka kundi la Dola ya Kiislamu ya Iraq na Sham (ISIL) kilionekana kuwa na udhibiti kamili wa mtambo huo ulio umbali wa kilomita 200 kutoka mji mkuu, Baghdad, na ambao hutoa robo nzima ya mafuta ya Iraq.

Afisa mmoja wa jeshi ameliambia shrika la habari la Ujerumani (dpa) kwamba sasa ni wanajeshi wa serikali walio kwenye eneo hilo, na hakuna uwezekano wa kurudi tena kwa ISIL. Hata hivyo, madai hayo bado hayajathibitishwa na vyanzo huru.

Mapigano ya kuwania udhibiti wa mtambo huo yamedumu kwa takribani wiki moja sasa, baada ya wanamgambo wa ISIL kuutwaa mapema mwezi huu. Tayari waasi hao wanadhibiti mji wa kaskazini wa Mosul na miji mingine midogo midogo kuelekea mji mkuu, Baghdad. Serikali inadai baadhi ya miji hiyo, lakini vyanzo kadhaa vya habari vinatilia shaka madai hayo.

Wito wa jumuiya ya kimataifa

Uwezo wa waasi kusonga mbele kirahisi umezua wasiwasi kwenye jamii ya kimataifa, huku sera ya Waziri Mkuu Nuri al-Maliki ya kuwapendelea Wairaqi wa madhehebu yake ya Shia na kuwadhalilisha wale wa Sunni ikikosolewa vikali.

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani akizungumza bungeni jijini Berlin.
Kansela Angela Merkel wa Ujerumani akizungumza bungeni jijini Berlin.Picha: picture-alliance/dpa

Ukosoaji wa hivi karibuni kabisa imetoka kwa Kansela Angela Merkel wa Ujerumani ambaye katika hotuba yake bungeni siku ya Jumatano amesema serikali ya Iraq imeshindwa kwa miaka kadhaa kujumuisha mitazamo ya makundi yote nchini humo.

"Tunahitaji serikali nchini Iraq ambayo inawakumbatia raia wote. Kwa miaka mingi, hilo halijatokezea na kwa sababu ya hilo, ndipo maana shinikizo linapaswa kuongezwa (dhidi ya serikali ya Iraq)." Amesema Kansela Merkel.

Nusra Front yajiunga rasmi na ISIL

Katika hatua nyengine, kundi la waasi wa Syria la Al-Nusra Front limetangaza kujiunga rasmi na ISIL, hatua ambayo sasa inaifungulia njia ISIL kuchukuwa udhibiti wa pande zote mbili za mpaka wa Iraq na Syria.

Wapiganaji wa kundi la ISIL.
Wapiganaji wa kundi la ISIL.Picha: picture-alliance/abaca

Mkurugenzi wa Shirika la Haki za Binaadamu la Syria lenye makao yake London, Rami Abdel Rahman, amesema kiapo cha utiifu kwa ISIL kilichotolewa leo katika mji wa Albu Kamal, kinakuja wakati ISIL ikisonga mbele katika jimbo la Deir Ezzor.

Awali, Nusra Front na ISIL walikuwa mahasimu, ingawa wote wana mafungamano na al-Qaida.

Nchini Iraq kwenyewe, wanamgambo wameishambulia kambi kubwa ya kijeshi katika mji wa Yathriib, ulio umbali wa kilomita 90 kutoka mji mkuu, Baghdad.

Wanamgambo wa ISIL wakisaidiwa na wapiganaji wa madhehebu ya Sunni waliizunguka kambi inayoitwa "Anaconda", mapema leo, na shirika la habari la Reuters linasema kiasi cha wapiganaji wanne wameuawa.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AP/Reuters/dpa
Mhariri: Mohamed Abdul-Rahman