1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iraq kupunguza mgao wa chakula

Mohamed Dahman28 Desemba 2007

Tangazo la serikali ya Iraq kwamba mgao wa chakula wa kila mwezi utapunguzwa kwa nusu limewafanya wananchi wengi wa Iraq wajiulize wataweza vipi kuendelea kuwa hai.

https://p.dw.com/p/ChIg
Watoto wa Iraq wakicheza kwenye kambi ya wakimbizi karibu na Najaf kusini mwa Iraq.Picha: AP

Serikali pia inataka kupunguza idadi ya watu wanaotegemea mfumo huo wa kugeiwa bure chakula kwa watu milioni tano ifikapo mwezi wa Juni mwaka 2008.

Mfumo wa mgao wa chakula nchini Iraq ulianzishwa na serikali ya S addam Hussein hapo mwaka 1991 kwa ajili ya kukabiliana na vikwazo vya kiuchumi vya Umoja wa Mataifa. Familia zilikuwa zikipatiwa vyakula muhimu kwa mwezi kutokana na kuanguka kwa uchumi na sarafu ya Dinar ya nchi hiyo.

Vikwazo hivyo vya Umoja wa Mataifa vilivyowekwa baada ya Saddam kuivamia Kuwait vilielezewa kuwa mauaji ya halaiki na Denis Halliday wakati huo akiwa mratibu wa misaada ya kibinaadamu ya Umoja wa Mataifa nchini Iraq.Halliday alijiuzulu wadhifa wake huo kupinga vikwazo hivyo viliokuwa vikiungwa mkono na Marekani.

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa vikwazo hivyo vimeuwa watoto wa Iraq nusu milioni,vimesababisha utapia mlo,magonjwa na uhaba wa madawa.Wairaq takriban wamekuwa wakitegemea moja kwa moja mgao huo wa chakula ili kuweza kuendelea kuwa hai.Mpango huo umeendelea hadi uvamizi ulioongozwa na Marekani nchini humo.

Lakini hivi sasa serikali inayoungwa mkono na Mrekani imetangaza kwamba itapunguza kwa nusu mgawo wa vyakula muhimu kwa sababu ya uhaba wa fedha na kupanda mno kwa gharama za maisha.

Upunguzaji huo ambao unatazamiwa kuanzishwa mapema mwaka 2008 umeshutumiwa sana kwamba serikali ya Iraq inashindwa kutowa mgao huo licha ya kuwa na mabilioni ya dola mkononi wakati Saddam Hussein aliweza kuundeleza mpango huo licha ya kuwa na dola zisizozidi bilioni moja.

Mohamed Hanoun katibu katika wizara ya biahara ya Iraq amekiambia kituo cha televisheni cha Kiarabu cha Al –Jazeera kwamba katika mwaka 2007 waliomba wapatiwe dola bilioni 3.2 kwa ajili ya mgao wa vyakula muhimu lakini kutokana na kupanda maradufu kwa bei za vyakula vinavyoingizwa nchini humo kutoka nje hapo mwaka jana wameomba kupatiwa dola bilioni 7.2 kwa mwaka huu ombi ambalo limekataliwa.

Wizara ya biashara hivi sasa inajiandaa kupunguza ruzuku ya orodha ya bidhaa kuu za chakula ambazo ni unga,sukari,mchele, mafuta ya kupikia na maziwa ya watoto wachanga.

Hatua hiyo itawaathiri takriban watu milioni 10 ambao wanategemea mfumo huo wa mgao wa chakula.

Wairaq wanaona mfumo huo wa mgao wa chakula wa kila mwezi ni msaada pekee kutoka serikalini na wa manufaa makubwa kwa familia ambao unajumuisha kilo mbili za mchele,sukari,sabuni ya kuogea na kufulia,majani ya chai,unga wa ngano,dengu na vitu vyengine kwa kila mtu.

Kwa mujibu wa repoti ya shirika la misaada la kimataifa Oxfam iliotolewa mwezi wa Julai mwaka huu asilimia 60 ya Waiarq hivi sasa wananufaika na mfumo huo wa mgao wa chakula idadi hiyo ikiwa imepunguwa kutoka asilimia 96 ya mwaka 2004

Repoti hiyo imesema kwamba asilimia 43 ya Wairaq wanaathirika na umaskini uliokithiri na kwa mujibu wa makadirio fulani zaidi ya nusu ya wananchi wa nchi hiyo hawana kazi, watoto ndio walioathirika zaidi kutokana na kupanda kwa gharama za maisha, viwango vya utapia mlo kwa watoto vimeongezeka kutoka asilimia 19 kabla ya uvamizi ulioongozwa n a Marekani hapo mwaka 2003 hadi kuwa asilimia 28 hivi sasa.

Wakati mishahara imeongezeka tokea kuvamiwa kwa nchi hiyo hapo mwaka 2003 imekuwa haiendi sambamba na ongezeko kubwa la bei za vyyakula na mafuta ya petroli.

Wairaq wengi wanahofu kwamba kupunguzwa kwa mgao huo wa chakula kunaweza kuzusha machafuko kwamba serikali itakuwa imefanya kosa kubwa kwa sababu mgao wa chakula cha kutosha unafidia mapungufu mengine ya serikali katika njanja nyengine kama vile usalama.