Iran yaualika ulimwengu kukagua mpango wake wa nyuklia
5 Januari 2011Serikali ya Iran imezialika Urusi, China, Umoja wa Ulaya na nchi nyingine kuvitembelea vinu vyake vikuu vya nyuklia, katika kuonyesha uwazi kwenye mpango wake, lakini mwaliko huo haukutolewa kwa Uingereza, Ufaransa, Ujerumani na Marekani, ambazo ni nchi zinazoupinga mpango huo wa nyuklia.
Mwaliko huo wa kushtusha wa Iran kwa mabalozi wa shirika la atomiki la Umoja wa mataifa mjini Vienna, umenuiwa kuonyesha uwazi katika mpango wa nyuklia wa Iran kabla ya mkutano na mataifa 6 yenye nguvu duniani, mjini Istanbul baadaye mwezi huu, kulijadili suala hilo.
Mataifa ya magharibi yanashuku mpango wa Iran wa kurutubisha madini ya Uranium unalenga kutengeneza silaha za nyuklia, huku Iran yenyewe ikishikilia kuwa ni mpango wa amani.
Marekani na Uingereza pamoja na wachambuzi wa magharibi, wanasema mwaliko huo hauna umuhimu wowote na wameiona hatua hiyo ya Iran kama ya kujipigia debe na kusema kuwa nchi hiyo itakuwa na uwazi iwapo tu itawaruhusu wakaguzi wa kimataifa kuvikagua zaidi vinu hivyo.
Hungary ambayo ndiyo nchi inayoshikilia wadhifa wa kupokezana wa Mwenyekiti wa Umoja wa Ulaya, imesema imealikwa. Mpaka sasa mkuu wa sera za nje wa Umoja huo Catherine Ashton ndiye ambaye amekuwa akiuwakilisha umoja huo katika mazungumzo ya Iran, na sio nchi mwenyekiti wa Umoja huo.
Kwa upande wa Marekani, msemaji wa wizara ya mambo ya nje, Philip.J.Crowley, amesema kwamba Marekani haikualikwa baada ya hapo awali Iran kusema kwamba ingeiruhusu kufanya ziara nchini humo.
Crowley amesema kuvitembelea vinu hivyo vya nyuklia vinavyojulikana na ambavyo vinatakiwa kukaguliwa na shirika la nishati ya atomiki, IAEA, hakutosaidia kuondosha shaka kwamba Iran ina dhamira ya siri ya kutengeneza silaha za nyuklia.
Crowley ameongeza kwamba hii ni mbinu ya kale ambayo Iran inatumia kuondosha shabaha kwa lililo muhimu, na kuwa ziara hiyo haiwezi kuliweka kando jukumu la nchi hiyo, ambalo ni kushirikiana kikamilifu na kwa uwazi na shirika hilo la atomiki, IAEA.
Baraza la usalama la Umoja wa mataifa, limekuwa likiiwekea Iran vikwazo mara kwa mara, kufuatia kukataa kwake kusitisha urutubishaji wa madini hayo ya Uranium, na kuwa na uwazi kuhusu shughuli zake za kinyuklia.
Mwandishi :Maryam Abdalla/RTRE/DPAE
Mhariri:Josephat Charo