Iran yatishia kujitoa katika makubaliano ya kinyuklia
29 Agosti 2018Amesema hayo kutokana na mataifa yenye nguvu ya Ulaya hivi sasa yanakabiliwa na kitisho kufuatia kujitoa kwa Marekani katika makubaliano hayo, na kusema Iran huenda ikajitoa pia katika makubaliano hayo.
Khamenei amemtahadharisha rais Hassan Rouhani kutotegemea mno uungwaji mkono wa mataifa ya Ulaya wakati akijikuta katika mbinyo mkali nyumbani kuhusiana na jinsi anavyoshughulikia changamoto za kiuchumi baada ya Marekani kurejesha vikwazo dhidi ya nchi hiyo, na mawaziri muhimu wakishambuliwa bungeni.
Kufuatia kujitoa kwa rais wa marekani Donald Trump kutoka katika makubaliano ya kimataifa ambayo yangedhibiti dhamira ya Iran kujipatia silaha za kinyuklia, mataifa yenye nguvu ya Ulaya yamekuwa yakitapia kuhakikisha kwamba Iran inaendelea kupata manufaa ya kiuchumi yanayohitajika ili kuibakisha katika makubaliano hayo ya kinyuklia.
Lakini katika matamshi yake yaliyochapishwa katika tovuti yake rasmi Khamenei alimwambia Rouhani na baraza lake la mawaziri leo, kwamba hakuna matatizo kuendelea na majadiliano na kuendelea na mahusiano na Ulaya, lakini anapaswa kuondoa matumaini kwao kuhusiana na masuala ya kiuchumi ama makubaliano ya kinyuklia.
"Makubaliano ya kinyuklia ni njia , sio lengo, na iwapo hatutafikia hitimisho hili , tunaweza kujitoa," Khamenei alinukuliwa akisema. Khamenei aliweka masharti kadhaa mwezi Mei kwa mataifa yenye nguvu ya Ulaya iwapo yanataka kuiweka Tehran katika makubaliano hayo.
Masharti ya Khamenei
Masharti hayo ni pamoja na hatua za benki za Ulaya kulinda biashara na Tehran na uhakikisho wa mauzo ya mafuta ya Iran.
Akizungumza katika mkutano huo leo, Khamenei alisema Tehran haitafanya majadiliano na maafisa wa marekani wasio na heshima na wanaopendelea mivutano " kufikia makubaliano mapya kuhusiana na mpango wake wa kinyuklia kwasababu Marekani inataka kujisifu kwamba wameweza kuileta Iran katika meza ya mazungumzo".
Khamenei amemwambia Rouhani na baraza lake la mawaziri kufanyakazi , "usiku na mchana " kutatua matatizo yanayoengezeka ya kiuchumi ambayo ni pamoja na kuporomoka kwa sarafu ya rial na kuongezeka kwa ukosefu wa ajira.
Lakini wakati huo huo ameonekana kulitaka bunge kutoweka mbinyo mkubwa zaidi dhidi ya Rouhani ambaye alihojiwa kwa kiasi kikubwa kuhusiana na utendaji wake kuhusu uchumi. Maafisa wanapaswa kujiunga pamoja dhidi ya mbinyo wa Marekani ambao , alisema , kwa kuwa kutangaza kuwapo na tofauti kutalifanya taifa hilo kutokuwa na furaha zaidi.
Wakati huo huo mawaziri kadhaa wa serikali wanatarajiwa kufika mbele ya bunge la Iran katika siku zinazokuja wakati wabunge wanadai majibu katika mzozo wa kiuchumi wa nchi hiyo.
Ufaransa nayo imewaambia wanadiplomasia wake pamoja na maafisa wa wizara ya mambo ya kigeni kuahirisha moja kwa moja safari ambazo si lazima kwenda Iran, ikielezea kuhusu mpango ulioshindwa wa shambulio la bomu pamoja na kuongezeka msimamo mkali wa Tehran kuielekea Ufaransa, kwa mujibu wa waraka wa ndani katika serikali ya Ufaransa.
Mwandishi: Sekione Kitojo / dpae
Mhariri: Iddi Ssessanga