1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran yataka uhakikisho wa hatima ya makubaliano ya kinyuklia

Sekione Kitojo
16 Mei 2018

Iran haitasalimu amri kutokana na mbinyo wa Marekani, amesema rais wa Iran Hassan Rouhani leo(16.05.2018), siku moja baada ya Marekani kuweka vikwazo vipya kufuatia kujitoa katika makubaliano ya kinyuklia ya mwaka 2015.

https://p.dw.com/p/2xnho
Hassan Rouhani
Picha: picture-alliance/AP Photo/E. Noroozi

Haya yanajiri wakati nchi za Ulaya zilizosaini makubaliano kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran zikifanya juhudi kujaribu kuyanusuru. 

Iran imesema  leo  kwamba  vikwazo  vipya  vilivyowekwa   dhidi yake na  Marekani  ni  jaribio la  kuvuruga  juhudi  za  kuokoa makubaliano ya  kinyuklia  ya mwaka  2015 zinazofanywa  na mataifa  yaliyobaki  yaliyotia  saini  kufuatia  kujitoa  kwa  Marekani kutoka  mkataba  huo.

Bildkombo Donald Trump und Hassan Rohani
Rais wa Marekani Donald Trump wa Marekani (kushoto) na rais Hassan Rouhani (kulia)Picha: Getty Images/AFP/N. Kamm//A. Kenare

Wizara  ya  fedha  ya  Marekani  jana  iliweka  vikwazo dhidi  ya gavana  wa  benki  kuu  ya  Iran , watu  wengine  watatu  na  benki ya  nyingine  iliyoko  Iraq, wiki  moja  baada  ya  rais Donald Trump kuiondoa  nchi  yake  kutoka  katika  makubaliano  hayo  na  Iran yaliyotiwa  saini  na  mataifa  yenye  nguvu  kuzuwia  mpango  wake wa  kinyuklia.

Iran imevieleza  vikwazo  hivyo  kuwa  ni  kinyume  na  sheria  na imeonya  kwamba  iwapo  mazungumzo  ya  kuokoa  makubaliano hayo  yatashindwa, itaanza  tena  mpango wake  wa  kinyuklia katika kiwango cha  juu  zaidi  kuliko  hapo  kabla.

"Kwa  hatua  hizo  za  uharibifu , serikali  ya  Marekani inajaribu kushawishi  dhamira  na  uamuzi  wa  mataifa  mengine  yaliyobaki yaliyotia  saini  makubaliano  hayo  ya JCPOA," amesema  msemaji wa  wizara  ya  mambo  ya  kigeni  ya  Iran  Bahram Qasemi akinukuliwa  akisema na  shirika  la  habari  la  Iran Fars.

Symbolbild Kündigung Atomabkommen mit Iran durch USA
Mchoro unaoonesha kuvunjiwa kwa mkataba wa kinyuklia na Marekani na Umoja wa Ulaya ukipinga hatua hiyoPicha: Imago/Ralph Peters

Mchakato mpya

Mawaziri  wa  mambo  ya  kigeni  wa  Uingereza, Ufaransa  na Ujerumani  walikutana  mjini  Brussels jana  kuangalia  vipi wanaweza kuokoa  makubaliano  hayo  ya  kinyuklia bila  Marekani , lakini mataifa  hayo yanaonekana  kupata  mbinyo  mkali  kuhusiana  na vipi makampuni  yao  yanaweza  kuendelea  kufanya  biashara  na Iran  mara  Marekani  itakapoanza  kurejesha  vikwazo.

Waziri  wa  mambo  ya  kigeni  wa  Iran Mohammad Javad Zarif alisema  mkutano  wao  ulikuwa  mwanzo  mzuri, lakini  anataka kuona  uhakikisho ukifanyakazi.

"Tumeanza  mchakato , ambao  unahitaji  kufanyika  kwa  nguvu kabisa,  na  hatuma  muda  wa  kutosha. Tunahitaji  kufikia hatua fulani  ya  uhakika  ambao utahakikisha  mafanikio  kwa  Iran katika muda maalum  ambao  rais  alisema wiki chache  zilizopita. Tutaona iwapo dhamira  ya  kisiasa ambayo  imeelezwa  na  washiriki waliobakia  katika  mkataba  huo  wa  JCPOA  unaweza  kutafsiriwa katika  kufanyakazi."

Deutschland Bundestag Angela Merkel
Kansela wa Ujerumani Angela MerkelPicha: Reuters/H. Hanschke

Kansela  wa  Ujerumani Angela Merkel  amesema  kwamba  njia bora  ya  kushughulikia  wasi  wasi  wa  kimataifa  juu  ya  jukumu  la Iran  katika  kanda ya  mashariki  ya  kati  pamoja  na  mpango  wake wa  makombora ni  katika  utaratibu wa  makubaliano  ya  kinyuklia, hata  iwapo Marekani imejitoa.

Mwandishi: Sekione Kitojo / rtre

Mhariri: Gakuba, Daniel