Iran: Mataifa ya magharibi yatadhoofisha ushirikiano na IAEA
21 Novemba 2024Iran imeonya kuwa azimio lililowasilishwa na nchi za magharibi kulaani mpango wake wa nyuklia katika Shirika la Kimataifa la Nguvu za Atomiki (IAEA), litapunguza na kuvuruga ushirikiano kati ya shirika hilo na Tehran.
Mataifa ya Marekani, Ufaransa, Uingereza na Ujerumani yamewasilisha rasimu ya azimio linaloikosoa Iran kwa kukosa ushirikiano, ambalo linatazamiwa kupigiwa kura leo hii kwenye mkutano wa bodi ya magavana wa shirika hilo mjini Vienna.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, amesema hatua hiyo ya nchi za Ulaya itavuruga na kudhoofisha ushirikiano. Naibu waziri wa mambo ya nje wa Iran, Kazem Gharibabadi, amesema kupitia mtandao wa kijamii wa X, kwamba nchi hizo zinaitumia IAEA kama chombo cha kisiasa.
Mataifa ya Magharibi yanataka ripoti ya kina kutoka kwa mkuu wa IAEA Raphael Grossi ifikapo msimu wa machipuko mwaka ujao, na yanataka majibu ya kiufundi kuhusu mabaki ya urani yaliyoonekana katika maeneo mawili ambayo hayajaorodheshwa.
Mataifa ya Magharibi yanaishtumu Iran kutaka kuunda silaha za nyuklia, madai ambayo Tehran inayakanusha. Mnamo 2018, Marekani ilijiondoa kwenye makubaliano ya nyuklia na Iran ya 2015 na kurejesha vikwazo dhidi ya nchi, ambayo ilijibu kwa kuongeza urutubishaji wa urani hadi asilimia 60, ikizidi kiwango kilichoafikiwa chini ya makubaliano hayo cha asilimia 3.67.