Iran yasema iko tayari kuendelea na mazungumzo juu ya mpango wake wa nyuklia
19 Januari 2006Iran imetangaza kwamba iko tayari kuendelea na mazungumzo ya kuutanzua mzozo wa mpango wake wa nyuklia huku shinikizo la kimataifa dhidi ya serikali ya Tehran linaloitaka isitishe urutubishaji wa madini ya uranium likizidi. Msimamo huo mpya wa Iran umetangazwa na balozi wa nchi hiyo katika shirika la kimataifa la nishati ya nyuklia, Dr Ali Asghar Soltanieh. Soltanieh amesema mkutano mwingine utakaojadili tatizo hili utafanyika mjini Moscow nchini Russia hapo tarehe 16 mwezi ujao wa Februari.
Ulaya na Marekani zimefutilia mbali uwezekano wa kufanya mazungumzo mengine na Iran juu ya swala hili. Soltanieh amesisitiza msimamo wa nchi yake kwamba imekuwa ikizingatia mikataba ya nyuklia iliyosainiwa na akasema Iran imesitisha kurutubisha madini ya uranium. Amesema kitu ambacho Iran imeanza kukifanya chini ya uchunguzi wa shirika la kimataifa la nishati ya nyuklia ni utafiti.
Mjumbe huyo pia amesisitiza azma ya Iran kuanzisha tena urutubishaji wa madini ya uranium ikiwa itafikishwa mbele ya baraza la usalama la umoja wa mataifa. Mataifa ya magharibi yanahofu mpango huo wa Iran hatimaye utapelekea kutengeneza silaha za nyuklia lakini Iran inashikilia mpango huo ni wa matumizi ya kiraia.
Kuhusu mzozo huu wa Iran waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Bi Condoleezza Rice anasema, ´Umoja wa Ulaya umetangaza wazi kwamba wairan wamevuka mpaka kiasi kwamba bodi ya magavana wa shirika la kimataifa la nishtai ya nyuklia lazima ichukue hatua, ili Iran itambue kwamba jumuiya ya kimataifa haitavumilia msimao wake kinyume cha masilahi ya ulimwengu wote kwa ujumla. Iran haipaswi kuruhusiwa kuwa na silaha za nyuklia, wala kuendeleza nyenzo zitakazoiwezesha kutengeneza silaha za nyuklia.´
Waziri wa mambo ya kigeni waUjerumani, Frank Walter Steinmeier, amesema mzozo wa nyuklia wa Iran lazima utanzuliwe na shirika la kimataifa la nishati ya nyuklia na baraza la usalama la umoja wa mataifa huku akikataa wazo la kuendeleza mazungumzo na Iran.
Akiwa ziarani mjini Cairo Misri bwana Steinmeier amesema baada ya kukutana na waziri wa mambo ya kigeni wa nchi hiyo kwamba Iran imekuwa kikwazo cha mazungumzo kuendelea kufanyika. Amesema bado wanategemea suluhisho la kidiplomasia katika kuumaliza mzozo huo lakini ni lazima suluhisho hilo lifikiwe na shirika la kimataifa la nishati ya nyuklia na baraza la usalama la umoja wa mataifa.
Bwana Steinmeier amesema msimamo huo umeeleweka na Misri. Amesema licha ya mzozo huo, Iran huenda ikawa tayari kulijadili pendekezo la Russia kurutubisha madini yake ya uranium.
Naye kansela wa Ujerumani Bi Angela Merkel kuhusu mzozo huu amesema, ´Naamini tunatakiwa kufikiri hatua kwa hatua na muhimu kabisa tuonyeshe ishara kwamba Iran inahisi haipendwi na jumuiya ya kimaitafa inaposhindwa kutimiza majukumu yake na ahadi zake katika mikataba. Singependa kwa sasa kuzungumzia sana hali ya baadaye lakini ni muhimu sasa hatua ichukuliwe.´
Wakati huo huo Afrika Kusini imetoa mwito mazungumzo ya kuutanzua mzozo wa nyuklia wa Iran yaendelee kufuatia tisho la Marekani na umoja wa Ulaya kuishtaki Iran kwa baraza la usalama la umoja wa mataifa. Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na wizara ya mambo ya kigeni ya Afrika Kusini, serikali ya Johannesberg inaendelea kushirikiana na serikali husika na wanachama wa bodi ya magavana ya shirika la kimataifa la nishati ya nyuklia kutafuta mapendekezo yatakayoweza kulimaliza tatizo hili kabisa.
Taarifa iliyotolewa baada ya mazungumzo kati ya naibu waziri wa mambo ya kigeni wa Afrika Kusini Aziz Pahad na kaimu waziri wa mambo ya kigeni wa Iran Mehdi Mostafavi, inataka mazungumzo juu ya mzozo wa nyuklia yaendelee. Taarifa hiyo inataka pia mazungumzo hayo yazingatie haki, majukumu, wasiwasi na malengo ya washikadau wote.
Uingereza, Ufaransa na Ujerumani ambazo zimekuwa zikijaribu kupata hakikisho kwamba Iran haitatumia mpango wake wa nyuklia kutengeneza silaha za nyuklia, zimitisha kikao cha dharura cha shirika la kimataifa la nishati ya nyuklia tareha 2 mwezi ujao kufuatia hatua ya Iran kuanza utafiti wa urutubishaji wa madini ya uranium. Utafiti huo ulikuwa umesitishwa chini ya mkataba uliosainiwa kati ya Iran na umoja wa Ulaya mwaka wa 2003 na 2004.