Iran yasema haitazungumza na Trump mpaka aondoe vikwazo
27 Agosti 2019rais huyo wa Iran amesema bila hivyo mkutano kati ya nchi hizo mbili utakuwa tu fursa ya kupiga picha za pamoja na yeye hayuko tayari kwa hilo.
Hatua hiyo ya kubadilika mwelekeo yamekuja siku moja baada ya Trump kusema jana Jumatatu kuwa kuna nafasi nzuri viongozi hao wawili wanaweza kukutana kuhusiana na mkwamo wao wa kinyuklia baada ya hatua ya ghafla ya rais wa Ufaransa Emmanuel Macron kuingilia kati wakati wa mkutano wa mataifa yenye utajiri wa viwanda wa G7 , kujaribu kuzileta pamoja Marekani na Iran baada ya miongo kadhaa ya mzozo.
"Bila ya Marekani kuondoa vikwazo , hatutashuhudia maendeleo yoyote yenye manufaa," Rouhani alisema katika hotuba aliyoitoa kwa njia ya televisheni, leo , na kuongeza kuwa Marekani "inashikilia ufunguo" katika kile kitakachotokea baadaye.
"Bila ya Marekani kuondoa vikwazo na kuacha njia potofu iliyochagua, hatuwezi kushuhudia maendeleo yoyote ya maana. Maendeleo ya maana yako Washington."
Fursa ya mazungumzo
Mapema jana Jumatatu , Rouhani alieleza kuwapo kwake tayari kufanya majadiliano ili kujitoa kutoka katika mzozo huu kufuatia Marekani kujitoa kutoka katika makubaliano ya kinyuklia.
"Iwapo nitafahamu kwamba kwenda katika mkutano na kumtembelea mtu kutasaidia maendeleo ya nchi yangu na kutatua matatizo ya watu, sitaikosa fursa hiyo," alisema. "Hata kama uwezekano wa mafanikio si asilimia 90 lakini asilimia 20 ama 10, ni lazima tusonge mbele kuelekea fursa hiyo. Hatupaswi kupoteza fursa."
Rouhani pia alimtetea waziri wake wa mambo ya kigeni , Mohammad Javad Zarif , dhidi ya ukosoaji kutoka kwa wenye misimamo mikali kuhusiana na ziara yake ya kushitukiza siku ya Jumapili katika mji wa Ufaransa wa Biarritz, ambako viongozi wa kundi la mataifa saba tajiri walikuwa wanakutana. Rohani alisema.
"Tunataka kutatua matatizo lakini kwa kupitia njia za busara. Lakini hatuhitaji fursa za kupigwa picha. Iwapo mtu anataka kupigwa picha na Hassan Rouhani , hilo haliwezekani."
Televisheni kwa lugha ya Kiingereza nchini Iran ya Press TV ilitoa taarifa isiyoeleweka baadaye jana, ikikataa juhudi za Macron.
Macron alisema ana matumaini Trump na Rouhani wanaweza kukutana katika muda wa wiki kadhaa zijazo kwa matumaini ya kuyaokoa makubaliano ya mwaka 2015 ya kinyuklia na Tehran yaliyofikiwa na mataifa yenye nguvu duniani, lakini ambayo Marekani iliamua kujitoa mwaka jana.