Iran yasema haiyumbishwi na Marekani
26 Aprili 2018Makubaliano ya Nyuklia ya Iran yaliyofikiwa na Jumuiya ya Kimataifa pamoja na Iran yanazidi kuibua mjadala kufuatia kitisho cha Marekani cha kutaka kujiondoa katika makubaliano hayo. Iran,na Urusi zimesema hakuna sababu ya makubaliano hayo kufanyiwa marekebisho kama anavyodai rais wa Marekani Donald Trump.
Kinachojitokeza wazi katika suala la Nyuklia la Iran ni mvutano kati ya nchi zinazounga mkono makubaliano hayo ya Nyuklia yaliyotiwa saini 2015 na Marekani. Rais Trump anasema kwamba ikiwa washirika wake wa Ulaya hawatokaa chini kuziondoa zina anazoziita dosari kubwa katika makubaliano hayo kufikia tarehe 12 mwezi Mei kitakachofuatia ni hatua yake ya kukataa kuongeza muda wa kuilegezea vikwazo Iran kuhusiana na uzalishaji wa mafuta. Mkataba wa Nyuklia unaopingwa na Trump uliungwa mkono na Ufaransa,Ujerumani,Uingereza,Urusi na China sambamba na Iran yenyewe.
Ulifikiwa baada ya Iran kuziridhisha nchi hizo kwamba mpango wake wa Nyuklia hautotumiwa abadan kutengeneza silaha za maangamizi. Marekani inazidi kuzishinikiza nchi hizo za Ulaya kuibana zaidi Iran kwa kuufanyia mageuzi mkataba huo.Iran leo imesema haotokubali hata mara kuruhusu marekebisho katika mkataba huo. Inaungwa mkono na Urusi ambayo leo vile vile imesema haioni nafasi yoyote ya kutokea mabadiliko au nyongeza yoyote katika makubaliano ya Nyuklia ya Iran.
Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Urusi Maria Zakarova ametoa kauli hiyo leo wakati waziri wa mambo ya nje wa nchi hiyo Sergei Lavrov akijiandaa jumamosi kukutana na wenzake wa Uturuki na Iran mjini Moscow kujadiliana juu ya suala hilo la Iran pamoja na mgogoro wa Syria. Nchini Iran kwenyewe kiongozi wa juu kabisa Ayatollah Ali Khamenei ameyataka mataifa ya kiislamu kushikamana kuipinga Marekani akisema Iran haiwezi kuingiwa na unyonge kwa unyanyasaji wa Marekani.Khamenei ameshangiliwa akimkosoa rais Donald Trump aliyesema siku ya Jumanne wiki hii kwamba baadhi ya nchi katika Mashariki ya kati haziwezi kudumu hata kwa wiki moja bila ya ulinzi wa Marekani. Hiyo ni kauli ya Trump ambayo Khamenei ameitaja kama udhalilishaji mkubwa kwa nchi za kiislamu.
''Waislamu wanapaswa kukipinga kiburi,nchi za kiislamu zinapaswa kuyapinga maonevu yanayofanywa na Marekani na nchi nyingine duniani.''
Cheche za Khamenei zinakuja katika wakati ambapo mshauri wake wa ngazi ya juu nae kutowa kauli akisema serikali ya mjini Tehran haitokubali hatua yoyote ya kubadilishwa mpango wa Nyuklia huku nchi za Magharibi zilizoyaridhia makubaliano hayo zikiandaa makubaliano mengine mapya zikitaraji kumshawishi Donald Trump kuendelea kuyaunga mkono. Rais wa Ufaransa alitamka jumanne kwamba amejadiliana na Trump kuhusu mkataba mpya na Marekani na Ulaya zitayashughulikia maeneo yanayoleta wasiwasi kuhusu Iran zaidi ya mpango wake wa Nyuklia. Trump anaiona Iran kama nchi inayoongeza kitisho na ameahidi kushirikiana na nchi za kiarabu za Ghuba pamoja na Israel kuizima nchi hiyo kutanua ushawishi wake katika kanda hiyo. Waziri wa Ulinzi wa Israeli Avigdor Liberman ameapa katika mahojiano aliyofanyiwa leo kwamba atayazima majaribio yoyote ya Iran ya kutaka kuingia kijeshi Syria.
Mwandishi:Saumu Mwasimba
Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman