1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran yapuuzilia mbali onyo la Marekani

7 Februari 2017

Kiongozi mkuu wa  Iran Ayatollah Ali Khamenei amepuuzilia mbali onyo la Donald Trump linaloitaka Iran kusitisha  majaribio ya makombora, akisema rais huyo mpya wa Marekani ameonyesha "sura halisi” ya ufisadi wa Marekani

https://p.dw.com/p/2X7Lg
Iran Kritik an den US Wahlen
Picha: picture-alliance/AP Photo

Katika hotuba yake ya kwanza tangu kuapishwa Trump, Ayatollah Khamenei ametoa wito kwa Wairan kujibu vitisho vya Trump mnamo Februari 10, wakati wa maadhimisho ya mapinduzi ya kiislamu ya Iran ya mwaka 1979. Kheamenei amesema Trump amejaribu lakini ameshindwa kuwatisha Wairan.

Kwa mujibu wa tovuti yake, kiongozi huyo mkuu wa kidini nchini Iran aliuambia mkutano wa makamanda wa kijeshi kuwa Wairan wanamshukuru Trump kwa kuyafanya maisha yao kuwa rahisi kwa sababu ameonyesha sura halisi ya Marekani.

Ikulu ya White House nchini Marekani imesema jaribio la kombora wiki iliyopita halikukiuka moja kwa moja mkataba wa nyuklia uliosainiwa mwaka wa 2015 kati ya Iran na nchi sita zenye nguvu duniani, lakini linakiuka "nia ya mkataba huo”.

Katika matamshi yake yaliochapishwa  leo, Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Iran Mohammad Javad Zarif amesema Iran haitakubali kuyatathmini upya makubaliano ya nyuklia.

USA Donald Trump bei der Vereidigung von James Mattis
Trump alionya kuwa Iran inacheza na motoPicha: Getty Images/O. Douliery

Zarif  ameliambia gazeti la Ettelaat kuwa anaamini Trump atashinikiza kujadiliwa upya kwa mkataba huo. Lakini Iran na nchi za Ulaya hazitakubali.

Wakati wa kampeni yake, Trump aliahidi mara nyingi kuufuta mkataba huo wa nyuklia. Wakati Waziri wake wa Mambo ya Kigeni Rex Tillerson hajatoa wito wa kukataliwa moja kwa moja muafaka huo, amedokeza kutathminiwa upya kikamilifu. Khamenei, ambaye ni kiongozi wa kidini mwenye mamlaka ya mwisho nchini Iran, pia amesema Trump amethibitisha kile walichokuwa wakisema kwa zaidi ya miaka 30 kuhusu ufisadi wa kisiasa, kiuchumi, kimaadili na kijamii katika mfumo wa utawala wa Marekani.

Trump alijibu jaribio la kombora la Iran mnamo Januari 29 kwa kusema kuwa "Iran inacheza na moto” na akatangaza vikwazo vipya kwa watu binafsi na makampuni, baadhi vikiwalenga wanajeshi wa mapinduzi wa Iran.

Azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linalounga mkono mkataba huo linaihimiza Iran kuepukana na kufanya majaribio ya makombora yaliyotengenezwa kuwa na uwezo wa kubeba silaha za nyuklia, lakini haliiwekei wajibu wa kufanya hivyo.

Chini ya mkataba huo, Iran ilikubali kusitisha  mpango wake wa nyuklia na badala yake  nayo iondolewe baadhi ya vikwazo vya kiuchumi ilivyowekewa na Marekani, Umoja wa Ulaya na Umoja wa Mataifa.

Rais wa Iran Hassan Rouhani alisema leo kuwa, kinyume na mtazamo wa Trump, makubaliano  ya nyuklia yalizifaidi pande zote na huenda yakatumiwa kama njia ya moja wapo  ya kupunguza mvutano katika kanda hiyo ya Ghuba.

Mwandishi: Bruce Amani/RTRE
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman