1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran yapinga madai ya Marekani kuhusu Venezuela

2 Mei 2020

Iran imesema tuhuma za Marekani kwamba Tehran inaipelekea msaada Venezuela hazina msingi ila Marekani inatafuta msingi wa kuiandama tena nchi hiyo na Venezuela. Venezuela kwa sasa iko kwenye hali ngumu kiuchumi

https://p.dw.com/p/3bgzD
Iran venezolanischer Präsident Nicolas Maduro besucht Präsident Hassan Rohani
Picha: picture-alliance/AA/ABACA/Iran Presidency

Iran siku ya Jumamosi  imeyapinga madai yaliyotolewa na Marekani kwamba nchi hiyo inaipelekea msaada Venezuela kukabiliana na tatizo la upungufu wa gesi. Iran imesema madai hayo hayana msingi bila ya kuitaja moja kwa moja Marekani. Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Mike Pompeo wiki iliyopita alisema ndege mbili za Iran za shirika la ndege la Mahan zilisafirisha msaada usiojulikana kwa serikali ya Venezuela.

Waziri huyo alitowa mwito wa kuzuiwa kwa safari hizo za ndege na kuzitaka nchi nyingine kuzuia safari za ndege za shirika hilo la Mahan. Shirika la habari la Associated Press liliripoti mwezi uliopita kwamba shirika la ndege la Mahan Air lilipeleka shehena ya kemikali muhimu inayotumika kutengeneza gesi ili kusaidia kufufua mtambo wa usafishaji mafuta uliochakaa katika nchi hiyo ya Kusini Mwa Amerika ambayo iko katika hali mbaya ya mgogoro wa kiuchumi.

Türkei Ataturk International Airport in Istanbul Mahan Air A310
Picha: picture-alliance/Russian Look/L. Faerberg

Venezuela kwa muda sasa inakabiliwa na upungufu wa gesi licha ya nchi hiyo kuwa na hifadhi kubwa ya visima vya mafuta duniani.

Iran na Venezuela zote ni nchi ambazo ziko chini ya vikwazo vikali vya Martekani  na zimekuwa na uhusiano wa karibu sana katika kipindi cha miongo miwili iliyopita.

Waziri wa mambo ya nje wa Iran aliandika ujumbe wa Twitta unaosema kwamba kauli zisizokuwa na msingi zimetolewa ili kuandaa mazingira ya Marekani kuongeza shinikizo lake dhidi ya serikali ya Venezuela.

Lakini taarifa nyingine ilisema kwamba Marekani ina nia ya kuuvuruga mpango wa serikali ya Venezuela wa kufufua viwanda vya usafishaji mafuta. Kauli hiyo haikukulenga moja kwa moja madai ya Marekani au kufafanua kuhusu mazingira ya ushirikiano kati ya nchi hizo mbili Iran na Venezuela.

Präsident von Venezuela - Nicolas Maduro
Picha: picture-alliance/dpa/Prensa Miraflores/J. Zerpa

Utawala wa Trump unataka kuongeza shinikizo katika kampeini yake inayolenga kumuondowa madarakani rais Nicolas Maduro na kumuangalia  kiongozi wa upinzani Juan Guido kama kiongozi halali wa Venezuela. Marekani na nchi nyingine karibu 60 za ulimwengu zinasema Maduro anang'ang'ania madaraka baada ya uchaguzi wa mwaka 2018 unaotajwa na wakosoaji kuwa wizi,kutokana na wanasiasa wa upinzani kuzuiwa kugombea.

Utawala wa Trumo uliiwekea vikwazo vikali Iran baada ya kujiondowa katika makubaliano ya Nyuklia ya Mwaka 2015 yaliyofikiwa baina ya Iran na nchi zenye nguvu duniani ikiwemo Marekani yenyewe.

Mwandishi: Saumu Mwasimba

Mhariri: Amina Mjahid

 

DW Kiswahili | Saumu Mwasimba
Saumu Mwasimba Mhariri na mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya DW