Iran yapinga kuondolewa vikwazo hatua kwa hatua
3 Aprili 2021Nchi hizo mbili zilisema siku ya Ijumaa kwamba zitafanya mazungumzo yasio ya moja kwa moja mjini Vienna wiki ijayo na hatua hiyo itakuwa kama sehemu ya mazungumzo mapana yanayolenga kuufufua mkataba wa nyuklia uliofikiwa mwaka 2015 kati ya Iran na mataifa yenye nguvu duniani.
Wizara ya Mambo ya nje ya Marekani imesema lengo la mkutano huo litakuwa juu ya hatua za mpango wa nyuklia ambazo Iran inahitajika kuchukua ili kurudi kwenye kufuata makubaliano yaliyofikiwa.
Soma zaidi:Iran yaitaka Marekani iondoe vikwazo dhidi yake
Kwa upande wake Ufaransa umeitaka Iran kuonyesha nia ya kujenga katika mazungumzo hayo yasiyo ya moja kwa moja kati yake na Marekani. Waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa Jean-Yves Le Drian aliysema hayo katika mazungumzo yake kwa njia ya simu na mwenzake wa Iran Mohammed Javad Zarif.
Waziri wa Mambo ya nje wa Ufaransa Jean-Yves Le Drian amesema katika tarifa yake kwamba kwamba ameitaka Iran ijiepushe na ukiukaji zaidi wa ahadi za sasa za mpango wake wa nyuklia ili kuyasaidia majadiliano hayo ya wiki ijayo.
Wakati huo huo Iran imesema ina imani kuhusu mazungumzo zaidi juu ya makubaliano ya nyuklia na viongozi wa mataifa yalio na nguvu duniani yanayotarajiwa kuendelea kufanyika wiki ijayo mjini Vienna, Austria.
Kiongozi wa shirika la nishati ya atomiki nchini Iran Ali Akbar Salehi amesema wanakaribia kutoka kwenye mkwamo kwa sababu ajenda za majadiliano haziendeshwi kisiasa bali kwa kuzingatia masuala ya kiufundi na kimalengo zaidi.
Siku ya Ijumaa kulikuwa na mkutano kwa njia ya video kati ya Iran na mataifa matano yaliyobakia katika makubaliano hayo ya nyuklia ambayo ni China, Ujerumani, Ufaransa, Uingereza na Urusi. Wote walikubaliana juu ya mazungumzo hayo ya kuuokoa mpango wa nyuklia wa Iran na uwezekano wa Marekani kurejea katika makubaliano hayo.
Soma zaidi:Iran: Umoja wa Ulaya usuluhishe mzozo wa nyuklia
Makundi ya wataalamu watakutana mjini Vienna Jumanne wiki ijayo. Wawakilishi wa Marekani pia watahudhuria. Lengo la mazungumzo hayo ya katika mji mkuu wa Austria, Vienna ni kufikia makubaliano ndani ya miezi miwili, kulingana na afisa mwandamizi na Jumuiya ya Ulaya ambayo ni mratibu wa mpango huo.
Rais wa zamani wa Marekani Donald Trump aliiondoa nchi yake kwenye mkataba huo wa nyuklia mnamo mwaka 2018 na kisha kuiwekea tena vikwazo Iran, hali iliyosababisha nchi hiyo kukiuka baadhi ya vizuizi vya makubaliano ya nyuklia yaliyofikiwa. Rais wa Marekani aliyeko madarakani sasa Joe Biden anataka kuyafufua makubaliano hayo lakini Washington na Tehran zimekuwa zikipingana juu ya nani achukue hatua ya kwanza.
Vyanzo:/RTRE/DPA