Iran yaonesha ishara ya kubadilishana meli zilizokamatwa
24 Julai 2019Wakati huo huo kampuni inayoendesha meli ya Uingereza ya Stena Impero ambayo ilikamatwa na Iran siku ya Ijumaa imesema imefanya mawasiliano na wafanyakazi wa meli hiyo.
"Hatutaki kuwa na hali ya wasiwasi na baadhi ya mataifa ya Ulaya," Rouhani amesema katika matamshi aliyoyatoa katika mkutano wa baraza la mawaziri yaliyowekwa katika tovuti rasmi ya serikali.
Katika tamko linaloashiria wazi kuwa linailenga Uingereza, Rouhani alisema iwapo "wataacha vitendo ambavyo si sahihi walivyofanya, ikiwa ni pamoja na kile cha Gibraltar, jibu la Iran , "litakuwa sahihi kwa matendo yao.
Iran na Uingereza zimo katikati ya mkwamo mkubwa kuhusiana na maafisa wa Uingereza waliokamata meli ya mafuta ya Iran nje ya eneo la Gibraltar mapema mwezi Julai na hatua ya Iran kukamata meli yenye bendera ya Uingereza katika eneo la maji la ghuba wiki iliyopita.
Rouhani pia amesema Iran itakuwa wazi kufanya mazungumzo iwapo kutakuwa na hatua ya kusitisha mapambano katika vikwazo vya kiuchumi vya Marekani dhidi ya jamhuri hiyo ya Kiislamu.
Uhasama baina ya Iran na Marekani umeongezeka tangu mwaka jana wakati rais Donald Trump alipoiondoa Marekani kutoka katika makubaliano ya kinyuklia ya mwaka 2015 yaliyolenga kuizuwia Iran kuendeleza mpango wake wa kinyuklia na kuanza kuiwekea vikwazo.
Mazungumzo yanaendelea
"Katika hali hii baadhi ya nchi ni wapatanishi, licha ya kuwa binafsi mataifa hayo yanasema wao si wapatanishi na wanatoa tu mawazo yao," Rouhani alisema.
Kumekuwa na mawasiliano kutoka kila upande katika suala hili na tunaendelea na hilo," ameongeza.
Waziri mkuu wa Japan Shinzo Abe alifanya ziara nchini Iran mwezi Juni kwa mazungumzo yenye lengo la kupunguza hali ya wasi wasi kati ya Iran na Marekani.
Mapema mwezi huu rais wa Ufaransa Emmanuel Macron alimtuma mshauri wake wa ngazi ya juu wa diplomasia , Emmanuel Bonne, nchini Iran "kuweka pamoja mkakati wa kupunguza wasi wasi".
Japan na Ufaransa zimekataa kuwa zinafanya kazi ya upatanishi kati ya Iran na Marekani.
Waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani Heiko Maas yuko katika mawasiliano ya karibu na mwenzake wa Ufaransa na Uingereza , ikiwa ni pamoja na kuangalia uwezekano wa ujumbe wa pamoja na Ulaya katika eneo la ghuba , licha ya kuwa msemaji wake amesema bado ni mapema mno kusema ushiriki wa Ujerumani utakuwaje katika suala hilo.
Wakati huo huo idara ya ujasusi wa ndani nchini Israel imesema leo kuwa majeshi ya usalama ya nchi hiyo yamefichua juhudi za kiintelijensia za Iran kuwaandikisha Waisrael Waarabu na Wapalestina. Taarifa kutoka Shin Bet hazikutoa idadi ama utaifa wa watuhumiwa ama kusema iwapo wamekamatwa ama kufunguliwa mashitaka lakini imesema wanaoshukiwa kuwa wafanyakazi wa operesheni inayoongozwa na Iran wamegunduliwa katika miezi ya hivi karibuni.