Iran yamnyonga mtu wa pili kuhusiana na maandamano
12 Desemba 2022Jarida la mtandaoni la idara ya mahakama ya Iran, Mizan limeripoti kuwa nchi hiyo imemnyonga mtu wa pili kuhusiana na maandamano yaliyodumu kwa karibu miezi mitatu sasa.
Kwa mujibu wa jarida hilo, mtu huyo, Majidreza Rahnavard aliyehukumiwa adhabu ya kifo Novemba 29 kwa hatia ya kuwauwa kwa kisu maafisa wawili wa usalama na kuwajeruhi watu wengine wanne, alinyongwa hadharani katika mji wa Mashhad.
Jarida la mizan limesema Rahnavard alikamatwa tarehe 19 Novemba akijaribu kukimbilia nje ya nchi. Iran inakabiliwa na wimbi la maandamano lililochochewa na kifo cha Mahsa Amini, msichana wa miaka 22 kilichotokea akiwa mikononi mwa polisi wa maadili.
Hukumu ya kwanza ya kifo kutokana na maandamano hayo ilitekelezwa Alhamisi iliyopita, dhidi ya Mohsen Shekari, kijana wa miaka 23 aliyekutwa na hatia ya kufunga barabara na kuwajeruhi polisi. Kunyongwa kwake kulilaaniwa katika sehemu nyingi za dunia.