1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran yalegeza kamba kuhusu mpango wake wa Nyuklia

17 Mei 2010

Iran yakubali kutuma madini yake ya Uranium, Uturuki, kama hatua ya kumaliza uhasama kati yake na Mataifa ya Magharibi.

https://p.dw.com/p/NPqL
Rais wa Iran Mahmoud Ahmadinejad, amsalimia mwenzake wa Brazil Luis Inacio Lula da Silva, mjini Tehran.Picha: AP

Jukumu sasa limo mikononi mwenu. Hayo ndio matamshi ya Iran kwa Mataifa ya Magharibi baada ya Jamhuri hiyo ya Kiislamu kutia saini makubaliano ya kurutubisha madini yake ya Uranium nje ya nchi hiyo. Brazil na Uturuki ndio waliofanikisha makubaliano hayo ambayo yanaashiria kupiga hatua kubwa kwa Iran kumaliza ule mzizi wa fitina kati yake na Jumuiya ya Kimataifa kuhusiana na mpango wake wa nyuklia.

Huku taarifa za makubaliano kwamba Iran hatimaye imesalimu amri na kuridhia kuyatuma madini yake ya Uranium kurutubishwa nje ya nchi zikitanda mjini Tehran- kulikuwa na kimya kikuu mjini Washington. Marekani, na washirika wake kuhusiana na makubaliano yaliyoafikiwa kwa juhudi za Uturuki na Brazil.

No Flash Erdogan Lula da Silva und Ahmadinedschad in Teheran
Iran, Uturuki, na Brazil baada ya kutia saini makubaliano.Picha: picture alliance/dpa

Ingawa Brazil na Uturuki hazina kura za turufu katika baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, walijitolea mhanga kuwa watajaribu kupatanisha kuhusiana na kukwama kwa mazungumzo kati ya Iran na mataifa ya Magharibi- kuhusiana na suala la kurutubisha madini yake nje ya Iran.

Na ndipo Rais Lula da Silva wa Brazil na Waziri Mkuu wa Uturuki, Tayyip Erdogan, walipofunga safari hadi mjini Tehran kuzungumza na utawala wa Rais Mahmoud Ahmedinenaj. Na hawakuondoka mikono mitupu. Iran ikatangaza kwamba imekubali itayasafirisha madini yake ya Uranium kiasi cha kilo 1,200 hadi nchini Uturuki ili kurutubishwa na baadaye itumie katika utafiti wa kimatibabu.

Yukiya Amano / IAEA
Mkurugenzi mkuu wa IAEA, Yukiya Amano.Picha: AP

Iran ilikubali kwamba itaanza kuyatuma madini hayo katika mwezi mmoja ujao. Pia walikubali Shirika la Umoja wa Mataifa la kudhibiti silaha za Nyuklia litasimamia shughuli hiyo nchini Uturuki. Kwa upande wao, Uturuki sasa inasema kwa kuwa Iran imekubali masharti haya- hakuna sababu yeyote kwa baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuiwekea Iran vikwazo zaidi.

'' Makubaliano haya ambayo yametiwa saini na Iran, yanaonyesha wazi, Iran iko tayari kufungua milango ya mazungumzo'' alisema Waziri wa mambo ya nje wa Uturuki, Ahmet Davotuglu.

Rais Mahmoud Ahmedinajad, naye kwa upande wake, alisema wakati umewadia kwa Mataifa matano, wanachama wa kudumu wa barazala la usalama la Umoja wa Mataifa, yaani, Marekani, Uingereza, China, Japan, Ufaransa na Ujerumani, kuanza mazungumzo na Iran.

Mataifa haya yalikuwa yameikalia Iran kooni, kukubali pendekezo la Shirika la kudhibiti silaha za Nyuklia kutuma madini yake ya Uranium nje ya nchi hiyo ili kurutubishwa. Tehran ilikubali shingo upande, lakini baadaye ikabadili nia na kutaka mpango huo wa kubadilishana utekelezwe nchini humo.

Ni hapo ndipo mzizi wa fitina ulipoanzia- Iran hatimaye imekubali sharti la kuyatuma madini yake nje ya nchi kurutubishwa, swala kuu hata hivyo ni je Marekani itaukubali mpango huu uliofikiwa na Brazil na Uturuki.

Mwandishi: Munira Muhammad/APE; RTRE

Mhariri: Othman Miraji