Iran yakosoa azimio la IAEA
25 Septemba 2005Tehran:
Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Iran, Bw. Manouchehr Mottaki, amesema leo kuwa azimio lililopitishwa na Shirika la Nishati ya Atomiki Ulimwenguni (IAEA) linalotaka nchi hiyo ipelekwe kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa ajili ya miradi yake ya kinuklia siyo halali hata kidogo. Amesema kuwa serikali yake inafikiria jinsi ya kulijibu azimio hilo. Mottaki ameliambia Shirika rasmi la Habari la Iran (IRNA) kuwa Iran haitasalimu amri kuhusu miradi yake ya tekinolojia ya kinuklia na urutubishaji wa madini ya uranium kwa ajili ya matumizi ya amani kama vile inavyoruhusiwa na Mkataba wa Kupiga marufuku utengenezaji wa silaha za kinuklia (NPT). Bw. Mottaki, hata hivyo, amesema kuwa Iran iko tayari kutekeleza kikamilifu masharti ya Mkataba huo na haijafunga mlango wa mazungumzo. Azimio linasema kuwa Iran haitaadhibiwa iwapo itasitisha mradi wake wa kurutubisha madini ya uranium, itashirikiana kwa dhati na Wakaguzi wa IAEA na kurudi kwenye meza ya mazungumzo na Wawakilishi wa Umoja wa Ulaya.