Iran yakaribia kuendelea tena na mpango wa kurotubisha madini ya Uranium.
12 Mei 2005Shughuli za Iran za kurotubisha madini ya Uranium,zilitafsiriwa na Marekani na nchi za Umoja wa Ulaya kama mpango wa nchi hiyo wa kutengeneza silaha za kinyuklia kwa ajili ya matumizi ya kijeshi.Iran kwa ukande wake na kwa muda wote,imekuwa ikikanusha na kudai kuwa ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida,hususan nguvu za umeme.
Wataalamu wa shirika la kimataifa la nguvu za atomiki IAEA,wamesema kuwa,Iran ikifanya hivyo,basi itapelekea shirika hilo kuwasilisha kesi mbele ya baraza la usalama la Umoja wa mataifa kwa ajili ya vikwazo na mbinyu zingine za kimataifa dhidi ya nchi hiyo.
Shirika hilo la nguvu za atomiki,lilikuwa likitaraji kupokea wakati wote ule barua rasmi kutoka kwa serikali ya Iran,kwamba inaksudia kurejerea shughuli zake za kurotubisha madini ya Uranium ambazo zilikuwa zimesimama kufuatia mazungumzo ya hivi karibuni.
Kulingana na gazeti la kimarekani la Washington Post,tayari Umoja wa Ulaya kupitia nchi tatu muhimu yaani Ufaransa,Ujerumani na Uingereza,ziliionya Irani kwamba miaka miwili ya mazungumzo kuhusu suala hilo itakuwa imepotea bure kutokana na vizingiti ambavyo Irani itakuwa imeviweka yenyewe.
Katika barua ya pamoja ambayo mawaziri wa mambo ya kigeni wa nchi hizo tatu wamemtumia Hassan Rohani ambae ndiye mwenyekiti wa tume ya Iran kwenye mazungumzo, wamesema shughuli kama hizo bila shaka zikakomesha kabisa mazungumzo na kwamba Iran peke yake ndiyo itakumbwa na madhara,wakimanisha vikwazo vya kimataifa.
Marekani hadi sasa inashikilia msimamo wake kwamba Irani inao mpango wa kutengeneza silaha za kinyuklia,na hivyo kuhatarisha amani katika eneo zima la mashariki ya kati.Marekani imekuwa ikizisihi nchi zingine wanachama wa shirika la kimataifa la nguvu za atomiki kuishitaki haraka Iran mbele ya baraza la usalama la Umoja wa mataifa,ili vichukuliwe vikwazo.
Lakini kufuatia majadiliano,Iran ilikubaliana na Uingereza,Ufaransa na Ujerumani mnamo mwezi Novemba mwaka jana kusitisha mpango wake,na hivyo kuweka mazingira bora ya kuwezesha mazungumzo kuzidi kusonga mbele.Kulikuwa pia kumetolewa ahadi kwa Iran ikiwa itawachana na mpango wake.
Irani katika kufanya hivyo,ilisema inaonyesha nia njema ya kufikia mwafaka kuhusu suala hilo.Lakini Irani inalalamika kuwa mazungumzo yamezidi kuzorota.
Mwanadiplomasia mmoja wa Ulaya ambae hakutajwa jina lake,amesema kuwa Irani ilikuwa haijalifahamisha shirika la nguvu za atomiki kama imeamuwa kuendelea na shughuli zake katika kituo cha Isfahan.Lakini mmoja wa wajumbe wa Iran kwenye mazungumzo,Cyrus Nasseri,ameliambia shirika la habari la Ufaransa la AFP kwamba hivi sasa yu mjini Geneva makao makuu ya shirika la nguvu za atomiki kuzungumza juu ya suala hilo.
Makamu rais wa Iran akiwa pia mwenyekiti wa shirika la taifa la nguvu za atomiki Gholam Reza Aghazedeh,aliiambia televisheni ya taifa kwamba Iran iliamua kusimamisha,kwa hiyo haina haja ya kuomba ruhusa ya kuendelea.
Rushia yaonyesha kuinga mkono Irani.Afisa moja wa Rushia anayehusika na masuala ya ushirikiano wa kinyuklia,amesema kuwa hatua ya Iran ni halali na ya haki.Na kwamba haitoathiri hata kidogo mahusiano ya Rushia na taifa hilo la kiislamu.
Mvutano huo ukiwa unaendelea,kuna duru za kidiplomasia zinazosema kuwa,kuna uwezekano wa kukafanyika mazungumzo mengine mnamo wiki mbili zijazo kujaribu kuusuluhisha mzozo huo.