Iran yakaidi onyo la Marekani, yarusha kombora jipya
23 Septemba 2017Televisheni ya taifa ya Iran imerusha mkanda unaoonyesha kufyatuliwa kwa kombora hilo aina ya Khoramshahr, ambalo kwa mara ya kwanza lilionyeshwa katika gwaride la kijeshi Ijumaa mjini Tehran.
Mtangazaji hakusema kombora hilo lilirushwa lini, ingawa Ijumaa, maafisa walikuwa wamesema lingefanyiwa majaribio bila kuchelewa. Majaribio ya awali yaliyofanywa na Iran yalifuatiwa na vikwazo vya Marekani, na lawama kwamba ilikuwa ikikiuka misingi ya mkataba kuhusu mpango wake wa nyuklia, uliosainiwa mwaka 2015 kati ya Iran na mataifa sita yenye nguvu duniani.
Rais Donald Trump ametishia mara kadhaa kwamba anaweza kuyafuta makubaliano hayo kutokana na kuendelea kwa Iran kufanya majaribio ya makombora, akidai majaribio hayo yanalenga kuipa Iran ujuzi wa kiufundi wa kurusha kombora la nyuklia, pale muda unaoelezwa katika ibara za makubaliano hayo kuizuia Iran kufanya hivyo utakapomalizika mwaka 2025.
Trump kuamua hatima ya makubaliano kuhusu nyuklia ya Iran
Ifikapo tarehe 15 Oktoba, Trump anatazamiwa kuripoti mbele ya bunge, iwapo anaamini Iran inatekeleza upande wake wa makubaliano hayo, na ikiwa anadhani Marekani inayo maslahi katika kuendelea kuyazingatia makubaliano hayo.
Ikiwa Rais Trump atasema Marekani hainufaiki na makubaliano hayo, kauli yake itafungua njia kwa bunge la Marekani kuvirejesha vikwazo dhidi ya Iran, na hali hiyo itaashiria kusambaratika kwa makubaliano yenyewe. Jumatano iliyopita, Trump alisema tayari amekwishachukua uamuzi lakini bado muda wa kuutangaza hadharani haujawadia.
Pande nyingine zilizotia saini makubaliano hayo; Uingereza, Ufaransa, Urusi, China na Ujerumani na Umoja wa Ulaya, zimesema zinataka makubaliano hayo yaendelee kama yalivyo.
Rouhani asema Iran itaendelea kujiimarisha kijeshi
Iran imesisitiza kuwa imeheshimu upande wake wa makubaliano hayo, na hayo yamethibitishwa na Shirika la kimataifa la nishati ya atomiki, IAEA. Shirika hilo limesema makubaliano hayo hayana kipengele kinachogusa masuala mengine.
Katika hotuba yake mbele ya gwaride kubwa la kijeshi mjini Tehran Ijumaa, Rais wa Iran Hassan Rouhani aliapa kwamba Iran itaendelea na mpango wake wa kuunda makombora, bila kujali mfululizo wa maonyo kutoka Marekani.
''Sio kwamba tutaimarisha mpango wetu wa makombora, tutaboresha pia uwezo wa jeshi la anga, nchi kavu na majini'', Alisema Rouhani katika hotuba hiyo. Kamanda wa vikosi vya Walinzi wa Mapinduzi Jenerali Amir Ali Hajizadeh, amesema kombora lililofanyiwa majaribio linaweza kusafiri umbali wa km 2,000, likibeba vichwa kadhaa vya mabomu.
Mwandishi: Daniel Gakuba/afpe, rtre
Mhariri: Zainab Aziz