1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani kuiwekea tena vikwazo Iran

Yusra Buwayhid
6 Agosti 2018

Iran inajiandaa kuwekewa tena vikwazo vya kiuchumi na Marekani Jumanne. Marekani imesema vikwazo vitaendelea kuwepo hadi pale serikali ya Iran itakapojibadilisha. Wairan nao wamekuwa wakiandamana dhidi ya rais wao.

https://p.dw.com/p/32fuI
Bildkombo - Trump und Rohani

 Akiwa anaelekea Marekani, baada ya kukamilisha ziara yake rasmi ya nchi tatu za Asia ya Kusini-mashariki, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Mike Pompeo amesema hatua ya kuiwekea tena vikwazo jamhuri hiyo ya Kiislam ni nguzo muhimu katika sera ya mambo ya nje ya Marekani kwa Iran. Pompeo ameutaja uongozi wa Iran kuwa na watendaji wabaya, na kwamba Rais wa Marekani Donald Trump ana nia ya kuwabadilisha, ili iwe kama nchi nyingeni ya kawaida.

Awamu ya kwanza ya vikwazo dhidi ya Iran itaanza kutekelezwa Jumanne. Ni vikwazo ambavyo viliwahi kuondolewa wakati wa uongozi wa rais wa zamani wa Marekani Barack Obama, chini ya makubaliano ya kinyuklia ya mwaka 2015. Lakini rais wa sasa wa Marekani Trump, alijiondoa kutoka katika makubaliano hayo mwezi Mei. Vikwazo hivyo vitakayvowekwa Jumanne vitalega sekta ya magari, dhahabu na madini mengine nchini Iran.

Awamu ya pili ya vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran itaanza kutekelezwa mnamo mwezi Novemba, ambavyo vitalenga sekta ya mafuta na benki kuu ya nchi.

Iran mfadhili wa ugaidi

Pompeo alibainisha kwa waandishi habari, kwamba kwa muda mrefu Marekani imekuwa ikiiangalia Iran kama kiongozi wa ufadhili wa makundi ya kigaidi, na kutokana na hilo Iran haistahili kupewa haki sawa kama nchi nyingeni yoyote na jumuiya ya kimataifa hadi pale itakaposita kujihusisha na shughuli za kigaidi.

Iran Demonstration in Karaj
Raia wa Iran wakiandamana, Karaj, Tehran dhdi ya serikali ya Rais Hassan RouhaniPicha: UGC

Wizara ya fedha ya Ujerumani kwa upande wake imesema Jumatatu kwamba itaendelea kuruhusu usafirishaji wa bidhaa zake nchini Iran pamoja na kutoa dhamana ya uwekezaji kwa makampuni yanayofanya biashara na Iran. Wizara hiyo imeongeza kwamba serikali ya Ujerumani bado inafanya mazungumzo na Marekani kuitaka iruhusiwe kuendelea na biashara na Iran na isiguswe na vikwazo hivyo vya Marekani.

Huku Iran ikiwa inajiandaa kukabiliana na vikwazo hivyo, maandamano ya raia wenye hasira dhidi ya Rais Hassan Rouhani na serikali yake yamezuka nchini humo.

Kumeshuhudiwa maandamano katika maeneo mbalimbali kwa siku kadhaa, yanayolalamikia uhaba wa maji, uchumi ulioporomoka pamoja na mfumo mzima wa kisiasa nchini humo.

Sarafu ya Iran yaporomoka

Mvutano unaoendelea Iran umeathiri pia sarafu yake, ambayo iliporomoka na kupoteza zaidi ya nusu ya thamani yake tokea mwezi April. Hali inayoongeza wasiwasi juu ya kiwango kikubwa cha ukosefu wa ajira, mfumuko wa bei pamoja na ukosefu wa mageuzi ya uongozi.

Rouhani anatarajiwa kutoa hotuba ya kitaifa kwa njia ya televisheni Jumatatu usiku, kuainisha mipango ya serikali yake ya kukabiliana na kuanguka kwa sarafu ya nchi pamoja na vikwazo itakavyowekewa na Marekani.

Mwandishi: Yusra Buwayhid/rtre/afp/ap
Mhariri: Gakuba, Daniel