1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran yaitaka Uingereza kuachilia meli yake mara moja

Admin.WagnerD12 Julai 2019

Iran imeitaka Uingereza kuiachilia meli ya mafuta ya jamhuri hiyo ya Kiislamu ambayo jeshi la wanamaji la Uingereza waliizuia wiki kwa madai ya kukiuka vikwazo vya Umoja wa Ulaya kwa kupeleka mafuta nchini Syria. .

https://p.dw.com/p/3Lyqz
Gibraltar - Patrouillenschiff der Royal Marine neben Supertanker Grace 1
Picha: picture-alliance/AP Photo/M. Moreno

Msemaji wa wizara ya nje ya Iran, Abbas Mousavi, ameliambia shirika la habari la nchi hiyo, IRNA, kuwa kitendo cha jeshi la Uingereza kilikuwa cha hatari na kitakuwa na athari zake kwa sababu hakuna sababu za kisheria za kuizuia meli hiyo. Ameishtumu Uingereza kwa kuzuia meli hiyo chini ya shinikizo la Marekani, akisema hatua hiyo ilichukuliwa kinyume cha sheria na huenda ikaongeza taharuki katika Ghuba ya Uajemi.Iran imeonya kuchukuwa hatua sawa na hiyo iwapo meli hiyo haitaachiliwa.

Hapo jana Uingereza ilisema kuwa meli tatu za Iran zilijaribu kuizuia meli inayomilikiwa na Uingereza iliyokuwa ikipita katika mlango bahari wa Hormuz, njia kuu ya usambazaji wa mafuta yanayotoka Ghuba kwenda katika maeneo mengine duniani lakini ikaondoa meli hizo baada ya kukabiliwa na meli ya kivita ya jeshi la wanamaji la Uingereza. Hata hivyo, waziri wa mambo ya nje wa Iran, Javad Zarif, amekanusha madai hayo, akisema si mara ya kwanza kwa Uingereza kutumia mbinu kama hizo kuficha uovu wake.

Iran Abbas Mussawi
Msemaji wa wizara ya nje ya Iran, Abbas Mousavi akiwahutubia wanahabari wa shirika la IRNA.Picha: Irna

Akihutubia kongamano la kitaifa la magavana hapo jana mjini Tehran, naibu rais wa kwanza wa Iran Es'hagh Jahangiri amesema kuwa Marekani na Uingereza ziliizuia meli hiyo iliyokuwa imebeba mafuta kutoka Iran baada ya kugundua kuwa Iran imepata suluhisho la kuuza mafuta yake. Ameongeza kuwa hatua hiyo inakiuka sheria za kimataifa na italeta aibu dhidi yao.

Maafisa wa polisi na idara ya forodha kwa usaidizi wa jeshi la wanamaji la Uingereza, walipanda na kuizuia meli ya  Grace 1 iliyokuwa ikibeba mafuta katika mlango wa bahari ya Gibraltar siku ya Alhamisi kutokana na ombi la Marekani. Baadaye siku hiyo, wizara ya mashauri ya nchi za kigeni ya Iran ilimtaka balozi wa Uingereza nchini humo Rob Macaire kueleza kuhusu pingamizi yake kuu kuhusiana na hatua hiyo. Aliambiwa kuwa hatua ya jeshi hilo la wanamaji la Uingereza inalingana na uharamia baharini.

Uingereza inadai kuwa meli hiyo ilikuwa ikipeleka mafuta nchini Syria iliyo chini ya vikwazo vya Umoja wa Ulaya  lakini Iran imekanusha madai hayo na kusema kwamba haiko katika uanachama wa Umoja wa Ulaya na pia haihusiki na vikwazo vyovyote vya mafuta vya Umoja wa Ulaya.