1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vikwazo vipya dhidi ya Iran vyaanza rasmi

5 Novemba 2018

Rais wa Iran Hassan Rouhani amesema nchi yake itaendelea kuuza mafuta yake na kukiuka vikwazo ilivyoekewa na Marekani katika sekta zake muhimu kama nishati na benki.

https://p.dw.com/p/37f3G
Persischer Golf Ölplattform
Picha: Reuters/R. Homavandi

Rais huyo wa Iran Hassan Rouhani, ameuwambia mkutano wa kiuchumi uliotangazwa  moja kwa moja kupitia televisheni ya kitaifa kwamba Marekani ilitaka kuzuwia mauzo ya mafuta ya Iran, lakini wataendelea kuuza mafuta hayo licha ya vikwazo walivyoekewa.

"Tumekuwa tukiuza mafuta yetu na tutaendelea kuyauza katika hali yoyote ile. Tuna haki ya kufanya hivyo. Wansema iran inakiuka vikwazo ndio tunasema wazi kwamba tutakiuka vikwazo vyenu ambayo havifai ni vya uonevu na vinavyokandamiza na vipo kinyume cha kanuni za kimataifa. Marekani itajuta.  Tutarejesha uekezaji wa kigeni humu nchini," alisema Hassan Rouhani.

UN-Generaldebatte: Macron und Rohani kritisieren US-Politik
Rais wa Iran Hassan RouhaniPicha: Getty Images/D. Angerer

Ijumaa iliopita  Marekani ilisema itaruhusu kwa muda mataifa manane yanayoagiza mafuta ya Iran kuendelea kununua mafuta hayo wakati itakapoiekea tena vikwazo Iran hii leo, vinavyonuiwa kuishinikiza nchi hiyo kuachana na mpango wake wa nyuklia, makombora na shughuli zake za kikanda. 

China, India, Korea Kusini, Japan na Uturuki, mataifa makubwa yanayoagiza mafuta kutoka Iran, ni miongoni mwa nchi hizo nane zinazotarajiwa kuendelea kununua mafuta ya taifa hilo la kiislamu ili kuhakikisha bei ya mafuta ghafi haiyumbi.

Kulingana na msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni ya Iran Bahram Qasemi, nchi yake bado inamawasiliano na mataifa mengine yaliotia saini mkataba wa nyuklia mwaka 2015. Amesema kwa sasa wanamikakati ya kuendelea na biashara na Umoja wa Ulaya, Qasemi ameongeza kuwa japo suala hilo linaonekana kuchukua muda lakini tayari wameanza kulifanyia kazi. 

Israel imepongeza hatua ya Marekani kuiwekea tena Iran vikwazo vya kiuchumi

Hata hivyo Israel kupitia waziri wake wa Ulinzi Avigdor Lieberman imepaza sauti yake juu ya hili na kusema kuwa hatua ya Trump ya kuiwekea tena vikwazo Iran ni ya kupongezwa na vitaleta mabadiliko yaliokuwa yakisubiriwa katika eneo la Mashariki ya kati. 

Avigdor Lieberman Archiv 30.06.2014 Berlin
Waziri wa Ulinzi wa Isarel Avigdor Lieberman Picha: Reuters

Israel imekuwa ikipinga vikali mpango wa nyuklia wa Iran na taifa sita yalio na nguvu duniani ikisema kuwa mkataba huo ulishindwa kudhibiti kitisho cha jeshi la Iran katika maeneo. 

Iran kuwekewa tena vikwazo ni moja ya mpango mkubwa wa serikali ya rais wa Marekani Donald Trump, kuilazimisha Iran kuachana na mipango yake ya nyuklia  pamoja na kujiingiza kwa taifa hilo katika mgogoro wa Yemen, Syria Lebanon, na katika maeneo mengine ya Mashariki ya kati. 

Mwezi Mei Trump aliiondoa Marekani katika makubaliano ya mpango huo wa nyuklia yaliotiwa saini mwaka 2015 na baadae Marekani ikaweka orodha ya kwanza ya vikwazo nchini Iran mwezi Agosti.

Mwandishi: Amina Abubakar/Reuters/AP 
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman