1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran: Wahudumu wa afya 10,000 waambukizwa COVID-19

Yusra Buwayhid
22 Mei 2020

Iran inakabiliwa na mripuko mbaya zaidi wa maambukizi ya virusi vya corona katika eneo la Mashariki ya Kati, huku wasiwasi pia ukizidi katika Ukanda wa Gaza na Yemen kutokana na ongezeko la idadi ya maambukizi hayo.

https://p.dw.com/p/3cb18
Iran Teheran Coronavirus
Picha: picture-alliance/AP Photo/A. Shirband

Virusi vya corona vimewaathiri wahudumu wa afya wapatao 10,000 nchini Iran, kulingana na taarifa za vyombo vya habari za jana Alhamisi zilizomnukuu Naibu Waziri wa Afya Qassem Janbabaei, ambaye hakufafanua zaidi.

Ripoti za mapema wiki hii, zimesema idadi ya wafanyakazi wa huduma ya afya walioambukizwa virusi hivyo ni 800 tu. Iran imesema zaidi ya watu 100 miongoni mwa wa wafanyakazi hao wamefariki. Iran ni taifa la Mashariki ya Kati linalokabiliwa na mripuko mbaya zaidi wa virusi vya corona, ambapo takriban watu 7,249 wamepoteza maisha kati ya watu 129,000 waliothibitishwa kuambukizwa virusi hivyo. Takwimu hizo ni pamoja na vifo zaidi ya 66 vilivyotangazwa Alhamisi na msemaji wa Wizara ya Afya, Kianoush Jahanpour.

Aidha, shirika la kimataifa la madaktari wasio na mipaka - MSF limesema idadi ya vifo vinavyohusiana na virusi vya corona katika kituo cha matibabu inachokishughulikia kusini mwa Yemen, inathibitisha kuwepo kwa janga kubwa nchini humo. Yemen ni taifa liloharibiwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe vya miaka mitano, na kusababisha janga la kibinadamu baya zaidi duniani.

WHO yakadiria janga kubwa zaidi Yemen

Shirika la Afya Duniani, WHO limesema makadirio yake yanaonyesha kwamba, nusu ya idadi ya watu wa Yemen wapatao milioni 30 inaweza kuambukizwa virusi hivyo na zaidi ya watu 40,000 wanaweza kufa.

Jemen | Corona Händehygiene in Slums
Yemen: Raia wakifundishwa jinsi ya kuosha mikono kujikinga na virusi vya coronaPicha: UNICEF/UNI324899/AlGhabri

Sehemu nyingine ya wasiwasi ni Ukanda wa Gaza, ambapo Wizara ya Afya imeripoti maambukizi mpya 35 katika siku tatu zilizopita na kuifanya idadi jumla ya watu waliopata maambukizi kufikia 55. Maambukizi yote mapya yamegunduliwa kwa watu waliorejea kutoka nchi za nje, ambao kwa lazima wamewekwa katika vituo karantini mpakani.  

Soma zaidiKipato duni kigezo cha kupata virusi vya corona

Mfumo wa afya wa Gaza umedhoofika sana kutoka na hatua ya Misri pamoja na Israel kufunga mipaka yao ya kuingilia katika ukanda huo, baada ya kundi la wanamgambo la Hamas kutwaa madaraka ya eneo hilo mnamo mwaka 2007. Ukanda wa Gaza unatajwa kuwa na mashine 60 tu za kupumulia pumzi katika eneo lenye idadi ya watu wapatao milioni mbili.

Kwa watu wengi, virusi vya corona husababisha dalili ndogo au za wastani, kama homa na kikohozi ambazo hupotea baada ya wiki mbili hadi tatu. Kwa wengine, haswa wazee na watu walio na matatizo ya kiafya virusi hivyo vinaweza kusababisha magonjwa mbaya zaidi, ikiwa ni pamoja na pneumonia au hata kifo.

Chanzo: ap