Iran na China zatafuta ufumbuzi wa mgogoro wa nyuklia wa Iran
1 Machi 2007Wakati huo huo China imekariri msimamo wake kuwa mgogoro huo unapaswa kupatiwa ufumbuzi kwa njia ya majadiliano.
Makamu wa waziri wa masuala ya nje wa Iran,Abbas Eraqchi amepanga kukutana na maafisa wa serikali ya China kuujadili mgogoro wa nyuklia.Ziara yake ya siku mbili mjini Beijing inafanywa huku Iran ikisema kuwa kamwe haitoachilia mbali mradi wa kurutubisha madini ya uranium kama inavyoshinikizwa na madola makuu.Siku moja kabla, madola makuu yalikubaliana kutayarisha mswada wa azimio jipya kuihimiza Iran kuchukua msimamo mwengine kuhusu mradi wake wa nyuklia.Wakati huo huo China inashikilia kuwa mgogoro huo utenzuliwe kwa njia ya kidiplomasia.Msemaji wa wizara ya nje ya China,Qin Gang hii leo alipozungumza na waandishi wa habari mjini Beijing alisema,ni matumaini ya China kuwa Iran itatia maanani wasi wasi wa jumuiya ya kimataifa na pia azimio 1737 lililopitishwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa hapo Desemba 23.Kuambatana na azimio hilo Iran ilipewa siku 60 kusita kurutubisha madini ya uranium au sivyo kukabiliwa na uwezekano wa kuwekewa vikwazo.Iran imepuuza wakati huo uliowekwa,kusistisha mradi wake wa kurutubisha uranium,ambao Marekani inadai kuwa ni sehemu ya mpango wa kutengeneza kwa siri silaha za nyuklia.
Hata hivyo,wajumbe wa nchi tano zilizo wanachama wa kudumu katika Baraza la Usalama,yaani Marekani,Ufaransa,Uingereza,Urussi na China zilipokutana pamoja na Ujerumani siku ya Jumatatu mjini London,zilisema kuwa zinataka kupata suluhisho la mgogoro huo kwa njia ya majadiliano. Urussi na China ni miongoni mwa madola makuu yanayopinga kufikiria kutumia nguvu au vikwazo vikali dhidi ya Iran,lakini hushiriki katika majadiliano yanayotafuta njia ya kuishinikiza Iran kusitisha mradi wake wa kurutubisha uranium. Wakati huo huo madola hayo yanaamini kuwa hatua kali dhidi ya Iran,zitazidi kuchochea mapambano.
Kwa upande mwingine,mkuu wa halmashauri ya masuala ya nje katika bunge la Urussi,Mikhail Margelov amesema,wakati wa ziara yake ya hivi karibuni nchini Iran hakuweza kupata majibu ya moja kwa moja kuhusu mradi wa kijeshi wa Iran.Kwa maoni yake alipozungumza na maafisa wa Iran,viongozi hao walikuwa wakijiepusha kujibu masuala yake.Amesema,ziara yake nchini Iran imeashiria kuwa mradi wa nyuklia wa nchi hiyo unaweza kubadilishwa kuwa mpango wa kutengeneza silaha.