Iran: Mpango wa sasa wa nyuklia utabaki kama ulivyo
30 Aprili 2018Rais wa Iran, Hassan Rouhani amemwambia Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron kwamba makubaliano kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran lazima yabaki kama yalivyo. Hayo yanajiri wakati ambapo Ufaransa, Ujerumani na Uingereza zimekubaliana kuunga mkono mpango huo wa nyuklia uliofikiwa mwaka 2015.
Taarifa iliyotolewa leo na ofisi ya rais wa Iran imeeleza kuwa Rouhani ameitoa kauli hiyo katika mazungumzo yake kwa njia ya simu na Rais Macron, ambapo amesisitiza kwamba Iran haitokwenda kinyume na majukumu ya sasa ya mpango wa nyuklia wa Iran na kwamba mpango huo na masuala mengine yoyote yale chini yake sio ya kujadiliwa kwa sasa.
Hata hivyo, Rouhani ameelezea utayari wake wa kujihusisha katika mazungumzo yatakayohusu masuala mengine, na ameongeza kusema kuwa Iran iko tayari kijadiliana ili kuhakikisha utulivu na usalama wa kikanda, hasa kupambana na ugaidi.
Uingereza, Ufaransa na Ujerumani wawanaunga mkono mpango wa nyuklia wa Iran
Rouhani ameuelezea mpango wa nyuklia wa Iran sio tu wenye kuijenga amani katika ukanda huo, lakini pia kama msingi wa uaminifu kati ya mataifa ya Magharibi na Iran. Kwa mujibu wa ofisi ya rais wa Iran, mazungumzo kati ya Rouhani na Macron yalidumu kwa muda wa saa moja.
Msemaji wa serikali ya Iran, Bagher Nobakht amesema kama mataifa ya Magharibi yanaonyesha nia ya kufanya mazungumzo na Iran kuhusu masuala ya mpango huo wa nyuklia, hilo ni jambo ambalo halipaswi kuzingatiwa kwa sasa.
''Iwapo hayo mazungumzo yatahusu masuala yetu ya ulinzi, hatutaki kujadiliana na mtu yeyote yule kuhusu masuala yetu ya kiulinzi na hatutoruhusu mtu yeyote atuwekee mipaka. Kwani sisi huwa tunawaambia Ufaransa na Marekani au wengine kile mnachopaswa kuheshimu kuhusu silaha zenu? Sasa kwa nini mtuwekee sisi mipaka?'' aliuliza Nobakht.
Makombora ya nyuklia ni miongoni mwa vipengele vitakavyojadiliwa
Hayo yanajiri wakati ambapo viongozi wa Uingereza, Ufaransa na Ujerumani wamerudia kuelezea nia yao ya kuunga mkono mpango wa nyuklia wa Iran, wakiuelezea kama njia bora ya kuondokana na kitisho cha Iran kuwa na silaha za nyuklia. Mwishoni mwa juma, Waziri Mkuu wa Uingereza, Theresa May, alizungumza kwa njia ya simu na Rais Macron pamoja na Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel ambapo kwa pamoja walikubaliana kwamba mpango wa sasa pia una vipengele muhimu ambavyo havikujumuishwa.
Viongozi hao wamesema vipengele hivyo ambavyo vinahitaji kujadiliwa ni pamoja na makombora ya nyuklia, kile kitakachotokea pindi mkataba huo utakapomalizika pamoja na hatua ya Iran kudhoofisha shughuli katika ukanda huo. Wameahidi kuendelea kushirikiana kwa karibu ili kuyalinda makubaliano hayo yaliyosainiwa mwaka 2015 kati ya Iran na mataifa yenye nguvu duniani.
Wiki iliyopita, Macron na Merkel walifanya mazungumzo na Rais wa Marekani, Donald Trump ambaye ametishia kujiondoa katika mpango wa nyuklia wa Iran uliosainiwa na mtangulizi wake, Barack Obama. Huenda Trump akatangaza maamuzi yake kuhusu mpango huo mwezi ujao wa Mei. Jana, mshauri wa masuala ya usalama wa ndani wa Marekani, John Bolton alisema kuwa Trump bado hajaamua iwapo aachane na mpango huo au la.
Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/DPA, AFP, Reuters
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman