1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran: Mpango wa makombora waweza kujadiliwa na Marekani

16 Julai 2019

Kwa mara ya kwanza, waziri wa mambo ya nchi za nje wa Iran Javad Zarif ameeleza kuwa mpango wa makombora wa nchi yake unaweza kujadiliwa na Marekani.

https://p.dw.com/p/3M8fy
Iran |  Mohammad Javad Zarif
Picha: ion

Iran imedokeza kuna uwezekano wa mazungumzo na Marekani kuhusu mradi wake wa makombora ya masafa ya mbali, ikiwa ni mara ya kwanza kwake kukubali kujadiliana juu ya silaha hizo, ingawa pia imeionya Marekani kuwa inacheza na moto. Haya yanakuja wakati Umoja Umoja wa Mataifa ukikosoa vikwazo vya usafiri vya Marekani vinavyolenga kumdhibiti waziri wa nje wa Iran, Mohammad Javad Zarif. 

Akizungumzia uwezekano wa kufanyika mazungumzo kati ya nchi yake na Marekani, Zarif aliweka sharti zito akisema kwamba lazima kwanza Marekani iache kuuzia Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu silaha. Nchi hizo mbili ni washirika wawili wakuu wa Marekani katika Ghuba.

Zarif alisema hayo wakati wa mahojiano yake na kituo cha televisheni cha NBC cha Marekani jana usiku. Alisema kuwa mwaka uliopita, Umoja wa Falme za Kiarabu ulitumia dola bilioni 22 na Saudi Arabia dola bilioni 67 kununua sialaha, nyingi kutoka Marekani, lakini Iran ilitumia dola bilioni 16 pekee.

Javad: "Marekani yacheza na moto"

Rais Donald Trump aliiondoa Marekani kwenye makubaliano kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran, mwaka uliopita.
Rais Donald Trump aliiondoa Marekani kwenye makubaliano kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran, mwaka uliopita.Picha: Imago Images/MediaPunch/R. Sachs

Akizungumzia kauli za Rais Donald Trump wa Marekani huku mvutano kati ya nchi hizo mbili ukiendelea kutokota kuhusu mpango ya silaha za nyuklia wa Iran, Zarif pia alionya kuwa Marekani inacheza na moto.

Hata hivyo, kwa Zarif kuzungumzia uwezekano wa mazungumzo kuhusu makombora ya nchi yake, ina maana kuna mabadiliko ya kisera. Mpango wa makombora ya Iran unasimamiwa na kitengo maalum cha askari wa mapinduzi wa Iran, na ambacho kiko chini ya kiongozi mkuu wa Iran, Ayatollah Ali Khamenei.

Kauli ya Zarif imejiri wakati Iran ikizidisha shinikizo lake lenyewe kuhusu mpango wake wa silaha za nyuklia baada ya Rais wa Marekani Donald Trump kuiondoa nchi yake kwenye mkataba huo mwaka uliopita.

Vikwazo vya usafiri dhidi ya Javad Zarif 

Katika tukio jingine, Umoja wa Mataifa umeelezea masikitiko yake kuhusu vikwazo ambavyo Marekani imeweka dhidi ya huyo waziri wa mambo ya nchi za nje wa Iran, wakati wa ziara yake jijini New York. Naibu msemaji wa Umoja wa Mataifa, Farhan Haq, amesema wameiandikia Marekani wasiwasi wao huo:

Vikwazo vinavyolenga kumdhibiti Javad zarif akiwa New York, vinamzuia kuzuru maeneo mengi ila tu majengo ya Umoja wa mataifa, uwanja wa ndege na ofisi za ujumbe wa Iran katika Umoja wa Mataifa na makaazi ya balozi wa Iran mjini New York.
Vikwazo vinavyolenga kumdhibiti Javad zarif akiwa New York, vinamzuia kuzuru maeneo mengi ila tu majengo ya Umoja wa mataifa, uwanja wa ndege na ofisi za ujumbe wa Iran katika Umoja wa Mataifa na makaazi ya balozi wa Iran mjini New York.Picha: Mojnews

"Ofisi inafahamu vikwazo vya usafiri ambavyo vimewekwa na Marekani kwa maafisa wa ubalozi wa kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa. Umoja wa Mataifa unawasiliana kwa karibu na ujumbe wa kudumu wa Marekani na Iran katika Umoja wa Mataifa kuhusu suala hili na umeelezea masikitiko yake kwa Marekani."

Zarif aliwasili jijini New York siku ya Jumapili na anatarajia kushiriki katika sehemu ya mkutano utakaofanyika kesho wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuhusu Uchumi na Masuala ya Kijamii (ECOSOC).

Vikwazo vipya vya Marekani vinavyolenga kumdhibiti Zarif, vinamaanisha maafisa wa Iran wanaweza tu kutembea katika majengo ya Umoja wa Mataifa, katika ofisi za mjumbe maalum wa Iran katika Umoja wa Mataifa, katika makaazi ya balozi wa Iran na kwenye uwanja wa ndege wa John F. Kennedy kumwezesha kusafiri nje ya nchi hiyo.